24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONTENA YA MAKONDA ‘HAYAUZIKI’

Na Grace Shitundu



Makontena 20 yenye samani za shule yaliyoingiza nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, yamekosa wateja kwa mara ya nne huku Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart ikiahidi kuendelea kutekeleza wajibu wa kuyauza.

Kampuni hiyo iliendelea kuyanadi makontena hayo katika ghala la Dar es Salaam Inland Container Deport (DICD)  eneo la Bandari Kurasini kwa idhini walioyopewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Mnada huo uliofanywa jana ulianza mapema saa tatu asubuhi kwa kunadiwa makontena hayo na mengine yaliyokuwa na vifaa vingine vilivyokuwa vikiuzwa kama matrekta, vifaa vya kilimo na magari.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastica Kevera, alisema pamoja na wateja kushindwa kufika bei kwa mara ya nne lakini wataendelea kuyanadi hadi hapo yatakapopata wateja.

 

“Utaratibu uliopo ni kuendelea kuyauza hadi yatakapofika bei inayohitajika na Serikali, kwa sasa wateja hawafiki bei, kwa sababu kama ulivyoona leo (jana) bei ya juu waliyofika kwa makontena haya ya samani ni shilingi milioni 25.

“Kiasi hicho bado wanakuwa hawajafika, hata hivyo tunapokuwa katika mnada kunakuwa na watu wa TRA ambao wenyewe wanaona hali ilivyo, sasa nini kifanyike Serikali ina mkono mrefu inaweza kujua cha kufanya,” alisema.

 

Pia alisema kazi ya kampuni yake ni kukusanya ushuru, kodi na kudai madeni kwa niaba ya TRA kwa kuwa wana mkataba nao.

Bei ya juu ya mnada wa makontena hayo iliyofikiwa na wateja ni Sh milioni 40 tangu yaanze kunadiwa.

Wiki iliyopita mmoja wa wateja waliofika katika mnada huo waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango walichokiweka endapo wanataka yanunuliwe.

Alisema kama kweli Serikali inataka kontena hizo zitoke basi washushe bei waliyoweka kwa sababu inaonekana kuna siasa zinazoingia katika mali hiyo.

“Sisi tunachoomba kama kweli wanataka kontena hizo zitoke washuke katika hiyo bei waliyoweka tutazichuku tu, lakini sasa naona kama zinaingia siasa katika hii mali,” alisema.

Kabla ya kuanza kwa mnada huo, Scolastika, alitoa masharti ya mnada huo kwa washiriki.

Mnada wa kwanza wa kontena hizo ulifanyika Agosti 25, mwaka huu na siku moja baadaye, Makonda, akiwa Ngara alifanya ibada maalumu ya kumuomba Mungu ili wanaofanya mnada huo wasipate wateja.

Makonda alishiriki ibada hiyo katika Kanisa la Anglikana iliyoongozwa na Mchungaji Sabimbona Rushashi, Mjini Ngara mkoani Kagera. “Amelaaniwa mtu yule atakayenunua furniture (samani) za walimu. Nimefanya ibada maalumu leo (jana) ya kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa sababu naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Dar es Salaam, wanaofanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi.

“TRA wameamua kuuza samani za walimu kwa wamiliki wa kumbi za starehe ili walimu waendelee kugombania madawati na vyoo na wanafunzi. Mimi Paul Makonda nimefanya kwa sehemu yangu kilichobaki ni mwenye wazo atasimama siku moja kujitetea,” alisema.

Mnada wa pili ulifanyika Septemba Mosi na watatu Septemba 8, mwaka huu hata hivyo wanunuzi waliofika katika mnada huo hawakufika bei pia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles