25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AORODHESHA MAFANIKIO DAR ES SALAAM

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema Serikali ya Awamu ya Tano haiungiungi mambo bali inatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nguvu zake zote.

Makonda alitoa akuli hiyo jana mbele ya viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, wakati akielezea tathmini ya mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho ndani ya mkoa wake.

Alisema utekelezaji wa ilani ya CCM ndani ya utawala wa Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, unakwenda vizuri kwa kadiri malengo yalivyopangwa.

Alisema ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa na mingi imekamilika ndani ya muda mfupi.

Akizungumzia ujenzi wa barabara, alisema mkoa anaouongoza una mtandao wa barabara wenye takribani kilomita za mraba 3,862.12.

Alisema mtandao huo umegawanyika katika sehemu mbili za utekelezaji ambazo ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura).

Alisema Tanroads wamesimamia kilomita 601 huku kilomita 3,260.91 zipo chini ya usimamizi wa halmashauri.

Alifafanua kwamba, kilomita hizo kwa  Wilaya ya Ilala ni 1,213, Kinondoni 611, Temeke 552, Kigamboni 626 na Ubungo 209.

Alisema kuwapo kwa mtandao huo wa barabara kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza foleni za barabarani ambapo siku za nyuma takribani Sh bilioni 400 zilikuwa zinapotea kwa mwaka.

Alisema katika ujenzi wa miundombinu kuna madaraja makubwa yanajengwa na mengine yapo kwenye mkakati wa kujengwa ambayo kusudio lake ni kuweka urahisi wa mawasiliano ya imara ya usafiri ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema ndani ya mkoa wake uwanja wa ndege ‘terminal three’ upo kwenye hatua ya mwisho ya kukamilishwa.

Alisema kukamilika kwa kiwanja hicho inamaanisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na viwanja vitatu ambapo kiwanja cha terminal three kitakuwa na uwezo wa kubeba watu milioni 6 kwa mwaka.

“Kukamilika kwa terminal three ina maana Tanzania kutakuwa ni njia panda ya ndege za mashirika mbalimbali duniani, hivyo maeneo ya Majumba Sita huko tunafumua na kujengwa mahoteli makubwa na hakika eneo hilo litabadilika sana,” alisema Makonda.

Alisema ujenzi wa reli ya Standard gauge unaendelea na kwa baadhi ya maeneo ndani ya mkoa wake reli hiyo itapita juu ili kupisha shughuli za wananchi.

Akizungumzia umeme, alisema kwa sasa nishati hiyo katika Mkoa wa Dar es Salaam ipo ya kutosha kiasi kwamba nishati nyingine wanaigawa kwa Mkoa wa Pwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles