SAADA SALIM, DAR ES SALAAM
Licha ya uongozi wa Azam FC kutangaza kusaka kocha mkuu wa kuifundisha timu yao hiyo lakini makocha wa Tanzania bado hawajawasilisha barua zao za maombi ya nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na kocha, Hans der Van Pluijm.
Majina ya makocha na CV zao yaliyopokelewa na uongozin wa Azam wakiwania nafasi hiyo nio 10 ambao ni raia wa kigeni na wane kati yao walishawahi kufundisha timu za hapa nchini akiwemo kocha aliyewahi kuifundisha timu hiyo, Aristica Cioaba.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC (CEO), Abdulkarim Amini (Popat), amesema hadi leo hawajapokea barua wala CV ya kocha yeyote kutoka Tanzania ila wamepokea majina 10 ya makocha kutoka nje ya nchi akiwemo aliyewahi kuifundisha timu hiyo.
“Bado hatujachagua kocha wa kuchukua nafasi ya Pluijm lakini tumepokea maombi ya makocha 10, huku wanne walishawahi kupita Tanzania wakiwemo Cioaba, Goran Kopunovic, Mosses Basena aliyewahi kuifundisha Simba na Leonard Neiva aliyewahi kuwa msaidizi wa Marcio Maximo wakati alipokuwa akiifundisha Yanga.
“Kwa Cioaba kama atarudi ama la ni taarifa tu, kama ni kweli itajulika lakini kwa sasa tunaendelea na mchakato wetu baada ya kumalizika kwa ligi, lolote linaweza kutokea, kikubwa tunahitaji mwalimu atakayeendana na malengo yetu,” amesema Amini.@