MAKINDA AZILALAMIKIA HOSPITALI ZA SERIKALI

0
4

Na FLORENCE SANAWA -MTWARA

MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda, amesema lugha chafu zinazotolewa na wahudumu wa afya katika hospitali za Serikali, zinachangia wagonjwa kukimbia katika hospitali hizo.

Akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya madaktari bingwa mkoani Mtwara jana, Makinda ambaye pia ni Spika wa Bunge mstaafu, alisema hospitali nyingi za Serikali zinakosa wagonjwa kutokana na madaktari na wahudumu kukosa ukarimu kwa wagonjwa.

“Sielewi hivi ni kweli wahudumu wa afya hawajui kama wagonjwa ndio mtaji wao?

“Wagonjwa ndiyo mali kuliko mali nyingine, wale tunaowadai fedha nyingi kwa sababu ya ukarimu wao ndio wanaopata wagonjwa wengi kuliko sisi.

“Mkoa wa Mtwara una asilimia 19 ya wanachama wa CHF kwa sababu gharama zake si kubwa. Nimesikia hapa kwamba, wanakuwa wanachangia shilingi 10,000 na wanatibiwa watu sita akiwamo baba, mama pamoja na watoto wanne ambao wana umri wa chini ya miaka 18.

“Pamoja na kwamba mfumo huu ni mzuri, ubaya wake ni kwamba mwanachama wa CHF anatibiwa katika eneo ambalo amejiunga,” alisema Makinda.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NHIF, Mkoa wa Mtwara, Gideon Katondo, alisema wamepanga kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufikia idadi ya watu zaidi ya laki tatu waishio mkoani hapa.

“Kwa sasa, tuna jumla ya wanachama zaidi ya 66,000 ambao wamejiunga na mfuko wetu ambao ni sawa na asilimia 19 ya idadi ya watu zaidi ya laki tatu waishio mkoani Mtwara.

Naye Dk. Albert Olemali kutoka Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), aliwataka wananchi wa Mtwara watumie huduma zao katika kipindi chote watakachokuwa mkoani hapa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here