23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Makamu wa Rais awapa somo viongozi Afrika

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema ili Afrika iweze kuwa huru hakuna budi viongozi wa sasa kuandaa mazingira ya Afrika bora na salama.

Kauli hiyo aliitoa juzi jijini Kampala nchini Uganda katika mkutano wa Africa Now Summit 2019.

Alisema pamoja na majadiliano kadhaa kuhusu uchumi na uwezeshaji wa vijana, lakini pia mkutano huo umeangalia suala zima la ongezeko la watu na uelewa wa vijana katika maendeleo ya nchi zao, hasa wakati huu wa uchumi wa viwanda.

Samia alisema hali hiyo sasa inazitaka nchi za Afrika kuangalia mitaala ya elimu inayotolewa kama inakidhi mahitaji ya kisayansi na kiteknolojia.

“Lazima sasa tuangalie hii idadi ya watu isije ikawa chanzo cha kuleta vurugu katika nchi zetu, bali iwe chanzo cha nguvu kazi kujenga nchi zetu,” alisema Samia

Alisisitiza kuwa Afrika ya sasa inahitaji viongozi ambao hawajitazami wao bali wanatazama wananchi wao katika makundi yao kama vijana, wanawake na walemavu.

“Ili tuwe Afrika tunayoitaka, lazima tuwe na utawala bora. Lakini utawala kwenye maendeleo ya kisiasa, lakini pia kujielekeza kiuchumi.

“Nadhani kazi yetu kubwa sasa hivi ni kujielekeza hapo, kwenye siasa ambazo zitaleta utawala bora, lakini tutajipanga kuwaendeleza vijana kiuchumi,” alisema.

Samia alisema katika suala la maendeleo ni lazima bado nchi na nchi hasa za Afrika zimekuwa zikitofautiana.

Alisema suala la uhaba wa chakula, ukosefu wa ajira mkubwa, umasikini na kutofautiana bado limekuwa ni jambo ambalo linatakiwa kuwekewa mkakati na nchi za Afrika.

“Tunatumaini kuwa sisi hapa tuna uwezo wa kutoa mwanga juu ya matarajio tuliyonayo kwa Bara la Afrika lililobadilika mienendo ambayo ni pamoja kuwa na aina ya uongozi inayohitajika kufikia mabadiliko hayo.

“Tofauti na siku za nyuma, sisi leo tuna nafasi nzuri ya kufikia mabadiliko haya. Kote barani, vijana wetu, wanawake, sekta binafsi na wanasayansi wanajaribu sana kushinikiza maendeleo na kubadilisha maisha. Nini kinachohitajika ni uongozi unaobadilisha na kuunga mkono watu wetu ambao wameonesha kuwa mbele ya Serikali katika kusukuma hilo,” alisema.

Samia pia alikutana na kuzungumza na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na baada ya kikao hicho, alisema Tanzania na Kenya ni majirani.

Alisema pamoja na kuwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini wao kama nchi jirani lazima wahakikishe uhusiano wao unasimama imara na kukuza ushirikiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles