33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAKAMU MWENYEKITI NCCR-MAGEUZI AHAMIA CCM

NA AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi (Bara), Leticia Mosore na wanachama wengine watano wametangaza kukihama chama hicho na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kuridhishwa na kazi inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mosore, aliyejiunga na chama hicho mwaka 2010 akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema awali alikihama chama hicho na kujiunga na upinzani baada ya kutoridhishwa na utekelezaji wa ilani, uwepo wa rushwa na ukosefu wa maadili pamoja na kuguswa na hoja zilizosimamiwa na upinzani.

Alisema amefanya uamuzi wa kurudi CCM baada ya kuridhishwa na kipindi cha miaka miwili na nusu cha utawala wa Magufuli na ameona mabadiliko makubwa na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali.

“Mipango ya utekelezaji wa utendaji wa Serikali unatendeka kwa uwazi, ukusanyaji wa mapato ya Serikali ni mzuri hadi sasa hivi ndege imenunuliwa kwa kodi zetu, Serikali imedhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali kidogo zilizopo katika mambo ya msingi,” alisema Mosore.

Alisema pia amevutiwa na hatua ya Serikali ya kutekeleza miradi mikubwa ikiwamo ya reli ya kisasa ya standard gauge (SGR), ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, ongezeko la dawa hospitalini na ujenzi wa barabara.

Pia alisema anachukizwa na kitendo cha wapinzani kupinga kila jambo.

“Kwa sasa kinachonikera zaidi upinzani ni kupinga kila kitu hata mazuri, upinzani tunapinga tu wakati hayo ndiyo tulikuwa tunayasema yafanyike, kazi yetu kupinga tu mwisho hatueleweki tunataka nini,” alisema Mosore.

Pia alisema miongoni mwa sababu zilizomsababisha kukihama chama hicho ni kuchoshwa na taratibu nzima za uongozi wa juu wa Chadema na kutopewa umuhimu kulingana na cheo chake katika shughuli mbalimbali za chama.

Oktoba, 2015 akiwa NCCR-Mageuzi, Mosore aliwahi kusimamishwa uongozi  kwa madai ya kukiuka utaratibu kwa kushirikiana na CCM kukihujumu chama hicho, uamuzi huo ulitolewa baada ya  kikao cha viongozi wa wakuu wa chama hicho kilichokutana Septemba 22.

Wanachama wengine walijiunga na CCM ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Mchata Mchata, Katibu wa Jimbo la Segerea, Lilian Kitunga, Mwenyekiti wa Jimbo la Segerea, Yunice Nyamantange, Mjumbe wa chama hicho Jimbo la Segerea, Jussy Chacha na Vedeline Nicolaus, ambaye ni mjumbe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles