26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Makamba: Wanafunzi kuanza shule kwa miche ya miti

makamba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January Makamba amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia mwakani itatoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule za serikali na zile za binafsi atahitajika kufika shuleni na mche mmoja wa mti siku ya kuanza masomo ikiwa kama moja ya mahitaji ya msingi na kwa upande wa wanafunzi wa sekondari watapaswa kufika na miche mitatu wakati wa kuanza masomo.

Waziri Makamba ameainisha kwamba maelekezo yatapelekwa Wizara ya Elimu na TAMISEMI na moja ya mahitaji ya kupewa cheti cha kuhitimu ni kukabidhi miti iliyopandwa wakati mwanafunzi anaingia kuanza masomo hivyo atahitajika kutunza na kuhudumia miti hiyo kipindi chote cha masomo.

“Kuanzia mwakani kila Mwanafunzi wa darasa la kwanza akiripoti atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba na hatapewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake. Katika shule zenye maeneo madogo, miti hiyo itapandwa katika maeneo yatakayoelekezwa na Serikali za Vijiji na Mitaa. Kwa wanafunzi wa Sekondari, itakuwa hivyo hivyo lakini itakuwa miti mitatu.”

“Kuanzia tarehe 5-6 Novemba tumewaita Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti na Mameya Wote Arusha Kwa ajili ya kuwapa mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusiana na Hifadhi ya Mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji,” Waziri Makamba alisema.

Waziri Makamba ameyasema hayo wakati akishiriki zoezi la upandaji miti na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambapo aliongozana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Iringa. Waziri Makamba ametanabaisha kuwa lengo la kushiriki zoezi la upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe mahsusi na wa uhakika kabisa kwamba uhifadhi,usimamizi na utunzaji wa Mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndio sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.

Waziri Makamba ameainisha kuwa katika shule zenye uhaba wa maeneo yanayoweza kutumika kwa upandaji miti, maeneo mbadala yatakayoelekezwa na serikali za vijiji na mitaa.

Waziri huyo mwenye dhamana ya Mazingira amesema hili linafanyika ikiwa ni moja kati ya hatua mahsusi, stahiki na za maksudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuendana na mabadiliko ya tabia nchi hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 61 ya nchi yetu ipo katika tishio la kuwa jangwa.

Vilevile Waziri Makamba amesema kuwa kuanzia tarehe 5-6 Novemba Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti na Mameya wote watakutana Jijini Arusha Kwaajili ya kupata mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusiana na Hifadhi ya Mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji

Waziri ametumia kifungu cha sheria ya Mazingira Sura ya 191 ya mwaka 2004 kutoa maagizo hayo ambacho kinasema “waziri atakuwa msimamizi mkuu wa masuala ya mazingira na kwa mantiki hiyo atatoa miongozo muhimu ya sera ili kukuza, kulinda na kusimamia kiendelevu mazingira nchini Tanzania. Waziri anaweza kutoa miongozo ya jumla kwa wizaraza kisekta, idara za serikali, baraza, kamati ya taifa ya ushauri wa mazingira, jiji, manispaa, kamati ya usimamizi wa mazingira wa wilaya, wakala au asasi nyingine yoyote ya umma au binafsi, miongozo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutekeleza au kufanikisha yaliyoelezwa kwenye sheria hii.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles