24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makamba, Kinana waitikia wito

MAKATIBU wakuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba na Abdulrahaman Kinana, jana wameitikia wito wa kufika mbele ya Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili.

Viongozi hao, walipokewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula katika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba, Dar es Salaam.

Mapema jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally, alisema hakuna kiongozi mstaafu  miongoni mwa makatibu wakuu wawili walioandikiwa barua ya kuhojiwa na kukataa, kama ambavyo imekuwa ikiandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

Akizungumza katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho Lumumba, Dk. Bashiru alisema taarifa zilizoandikwa zikieleza kuwa makatibu wakuu wawili wastaafu, Makamba na Kinana wanaokabiliwa na tuhuma za kimaadili ndani ya chama hicho wameitwa na kukataa kwenda kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili si za kweli.

“Hakuna kiongozi yeyote ambaye amepelekewa wito na akakataa kuitikia wito, uongo. Huyo anajipenda hajipendi? Maana haya mambo ya kuitana hayajaanza leo. Watu huitwa, wengine kukaripiwa, wengine onyo kali, wengine kusamehewa, wengine kufukuzwa, tangu enzi za Tanu.

“Marehemu Mtemvu (Zuberi Mtemvu, miongoni mwa wanachama wa Tanu walioshiriki kupigania Uhuru wa Tanganyika) alikimbia Tanu akajifanya anajiuzulu, Tanu ikakaa kikao ikamfukuza, sijazaliwa mie wala Magufuli (Rais John Magufuli) hajazaliwa, kuna jipya gani?

 “Lakini unasikia makelele barabarani huko mpaka yaani sasa unafurahia hizo stori, maana yake unaona mtu mzima anaandika kwenye gazeti zito lenye heshima, wanashindwa nini kuja makao makuu hapa kunitafuta. Hakuna hata mwandishi wa habari mmoja aliyekuja ofisini kwangu ili nimpe uhakika wa mambo, wote wanaandika tu bila hata haya,” alisema Dk. Bashiru.

Alisema ni vyema waandishi wa habari wawe na subira wakipata taarifa.

“Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa chama mstaafu aliyewahi kuitwa kwa mashauriano kwenye vikao vya kikatiba akakataa, na kama wanalitarajia hilo, halijatokea kipindi hiki, halipo,” alisema Dk. Bashiru.

Alikuwa akizungumzia taarifa za mwishoni mwa wiki zilizoeleza kuwa makatibu hao wakuu wastaafu, walitakiwa kuhojiwa Ijumaa wiki iliyopita, lakini hawakufika na badala yake waliandika barua za kujiondoa uanachama.

Hata hivyo, mmoja wa watuhumiwa katika suala hilo, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ambaye pia aliwania kupitishwa na CCM kuwania urais mwaka 2015 bila mafanikio, aliitwa na kuhojiwa na kamati hiyo Alhamisi iliyopita.

SUMAYE AREJEA CCM

Katika hatua nyingine, Dk. Bashiru pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Mali za CCM, mama Anna Abdallah, naibu makatibu wakuu wa CCM, Tanzania Bara na Visiwani, wamempokea rasmi Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye ametangaza kurudi kwenye chama hicho.

Sumaye ambaye alipokewa ofisi ndogo ya CCM-Lumumba, alipokwenda kujiunga tena na chama hicho, alisema Tanzania hakuna vyama vya upinzani vyenye malengo ya kuchukua dola na kwamba kwa kipindi chote alichokuwa upinzani, ni kama alikuwa amebeba maji kwa kutumia gunia.

Pia aliwatahadharisha Watanzania kuwa vyama vya upinzani vilivyopo ni vyama masilahi na ndiyo maana wao kila kukicha kazi yao kubwa ni kugombana na Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Sumaye alisema aliondoka CCM kwenda kujenga upinzani imara, lakini matarajio yake yamekuwa tofauti, akidai alikuwa katika sehemu ambayo amebeba maji kwa kutumia gunia.

 “Niliondoka kwa kuwa nilikuwa na dhamira ya kuwa na chama imara cha upinzani chenye mwelekeo wa kuchukua dola, lakini yaliyopo kule ni hatari, na niwaeleze Watanzania kuwa CCM ndio chama bora na chenye fikra za kumkwamua mwananchi.

“Nilikwenda kujenga upinzani, ila kwa nilichokikuta huko, kazi kubwa ni kupambana na Polisi na Usalama wa Taifa, hawana ajenda nyingine, hakuna upinzani, dhahiri ni upinzani masilahi.

“Ninaomba mnipokee ndugu zangu na ninaahidi kushirikiana kwa moyo mkunjufu, na Watanzania wananijua huwa sina unafiki.

“Baada ya kuhangaika na hawa jamaa zangu, nikaona kwa kweli nabeba maji kwa gunia, faida pekee ni kuloana mgongo tu,” alisema Sumaye.

Akizungumzia ujio wa Sumaye, Dk. Bashiru alisema watapanga siku na nafasi zaidi ya kumpokea, ambapo tawi lake la chama ni Makao Makuu Dodoma, ambako zitafanyika taratibu pamoja na kupeleka salamu kwa Mwenyekiti wa chama, Rais Dk. John Magufuli katika kikao cha Kamati Kuu kinachotarajia kufanyika kesho.

Dk. Bashiru alisema wanampokea Sumaye kwa mikono miwili kwa kuwa ni kiongozi mkubwa na mwenye mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa la Tanzania kwa kuwa alikuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka 10 katika utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Spika mstaafu wa Baraza la Uwakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, ambaye sasa ni mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Mali za CCM, alisema Sumaye ni mali iliyopotea awali na sasa wameirudisha, wanampokea kwa mikono miwili na wanamkaribisha kwa kuwa ni mtu mkweli.

“Nilifanya kazi na Sumaye akiwa Waziri Mkuu, ni mtu mkweli na mwenye kutoa ushirikiano kila unapomuhitaji, hivyo kurudi kwake atakuwa msaada mkubwa kwetu na tunampokea kwa mikono miwili ndani ya CCM,” alisema Kificho.

HISTORIA YA SUMAYE

Sumaye alizaliwa Mei 29, 1950 na alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Novemba 27, 1995 hadi Desemba 28, 2005 katika Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Akiwa mwanachama wa CCM, aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Hanang kwa miaka 22, kuanzia mwaka 1983 hadi 2005.

Kabla ya kuwa Waziri Mkuu, alihudumu kama Waziri wa Kilimo, Mifugo na Ushirika katika Serikali ya Awamu ya Pili iliyokuwa chini ta Rais Ali Hassan Mwinyi, aliyeongoza kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.

Baada ya kutoka madarakani, kuanzia mwaka 2006 Sumaye alirejea shuleni baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard, kupitia programu ya Edward S. Mason kwenye shule maalumu ya John F. Kennedy iliyopo chuoni hapo nchini Marekani, na alipata shahada ya juu katika Usimamizi wa Umma (Public Administration).

Alirejea nchini baada ya kumalizia masono yake na mwaka 2015 alijitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika kiti cha urais, lakini hakufanikiwa.

Agosti 22, 2015, alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai kuwa anakwenda kuimarisha upinzani ili uweze kuchukua dola na kuimarisha demokrasia nchini.

Desemba 4, mwaka jana aliondoka Chadema kwa kile alichodai kutoridhika namna ya siasa za chama hicho zinavyoendeshwa kwa kuminywa kwa demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles