23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makamba amjibu Mokiwa, JK

Januari Makamba
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema hawezi kubishana na Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa, kwa sababu ni kama baba yake.

January aliyasema hayo jana wakati akizungumza na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam.

January ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga (CCM), alisema iwapo Askofu Mokiwa kwa mtazamo wake anaona staili ya unyoaji nywele ni sifa ya urais basi anawaachia waumini wake na Watanzania kupima wenyewe kauli hiyo.

Mbali na Mokiwa pia January alitumia nafasi hiyo kujibu kauli ya Rais Kikwete ambaye alimpa ushauri wa kusikiliza ushauri wa wazee kabla ya kufanya uamuzi wake.

“Wako wazee wengi ndani ya CCM wa kuwaona na wengine nimekwishawaona na Rais Kikwete kwa nafasi yake ni refarii wa mchezo,” alisema January.

Alisema kutangaza kwake kugombea si kwamba anataka cheo cha urais kwani kwake urais ni utumishi.

January alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Askofu Mokiwa kuzungumzia sifa za mgombea urais akisema nchi haiko tayari kuongozwa na wanyoa ‘unga’ (kipara) na kwamba wakati wa Tanzania kuongozwa na vijana haujafika.

Ingawa Mokiwa hakutaja moja kwa moja jina la January, lakini ndiye kijana pekee ambaye ametangaza nia ya kuwania urais na kudai ni wakati wa vijana kushika hatamu za uongozi.

Wasomi nao wamshauri

Baadhi ya wasomi nchini wamemtaka January kufuata ushauri aliopewa na Rais Jakaya Kikwete, asilazimishe kuwania nafasi ya urais kwa sababu wakati ukifika atapata.

Akiichambua kauli hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema haiwezekani kwa mtu kupewa nafasi ya uongozi kama hana uzoefu wa kazi.

Dk. Bana alisema kutokana na hali hiyo ndio maana hata, Rais Kikwete alitengenezewa njia kabla ya kupewa jukumu la kuiongoza nchi.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Hajji Semboja alisema kauli ya Kikwete ni ya kiongozi mwenye hekima na busara.

Alisema kila chama kina utaratibu wake wa kuchagua wagombea, hivyo alipaswa kufuata utaratibu huo kabla ya kutangaza hadharani.

Kauli ya Kikwete imekuja siku chache baada ya January kutangaza kuwania nafasi hiyo wakati akihojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), wiki iliyopita.

Habari hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta, Grace Shitundu na Veronica Romwald (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. CCM wana ubguzi, mbona walisema january kafungiwa kufanya siasa za kujitangaza pamoja na wenzake. Mbona hawajibishwi, hapa kuna kitu, Rais amekuwa mpole mno kwa sheria ambazo chama chake kinajiwekea. Sasa hii ni nini? Kusema tu Rais amempa ushauri haitoshi je wale wengineo nao watangaze basi. Ubaguzi katika utendaji hautakiwi katika uendeshaji wa siasa, na kila mwanasiasa CCM ataibuka na kusema Rais amenishauri, hivi kweli Rais atashauri au kuwapendekeza wagombea wangapi ndani ya CCM? CCM mwakani mnakazikubwa sana, ndo mwanzo wa kusambaratika chama huooooooooo..CCM HIYOOOOOOOOOOOOO!!!!!!!!!!!!!!! Inaishia, “hakuna jambo lisilokuwa na mwisho.”

  2. Mimi nadhani tungetafakari maneno mawili hapa “kutangaza” na “ujana.” January kalisema la urais ndani ya BBC kupitia mahojiano tu tayari inasemwa “katangaza.” Mimi nadhani alijibu swali aliloulizwa au labda amepima joto, na kweli amefanikiwa maana hata Rais tayari kaonessha “reaction,” nadhani haikuwa na haja kufanya hivyo. Hili la ujana nalo lina utata. Kuna Askofu mmoja aliteuliwa hapa miaka michache iliyopita. Askofu huyo akaitwa Askofu Kijana wakati akiwa na miaka 50. Kulingana na “life expectancy” ya nchi basi tungeliweza kusema Marekani walichagua Rais mtoto kwa maana Obama aliingia madarakani akiwa na miaka 47 wakati life expectancy Marekani iko juu sana ukilinganisha na Tanzania ambapo Kikwete alikataliwa kuwa Rais kwa kuwa alikuwa kijana wa miaka 45!Tuache kudhalilishana, mtu mwenye miaka 18 ni mtu mzima tayari, na akipita 35 anakuwa amekomaa akili ya kutosha kabisa kuwa kiongozi wa juu wa nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles