27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Majini ya rushwa bado yanamsumbua Mangula

philip-mangulaNA NISAKUMBONA KALULUNGA

WIKI iliyopita Makamu Mwenyekiti (Taifa) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, alinukuliwa na vyombo vya habari akiwaonya wanachama wa chama hicho ambao wameanza kujinadi kwa kutoa zawadi na rushwa kwa baadhi ya wanachama wenzao.

Madhumuni ya wanachama hao kufanya hivyo ni maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho ambao unatarajiwa kufanyika 2017 kwa ngazi zote za uongozi kuanzia mashina, matawi, kata, wilaya, mkoa na taifa.

Mangula ameendeleza matamko yake ambayo aliwahi kuyatoa hata mwaka jana kuwa watoa rushwa ndani ya chama hicho majina yao yangekatwa, huku akijinasibu kuwa kwa ngazi ya wagombea urais alifungua na makabrasha kwa ajili ya kuwashughulikia kimaadili wagombea urais.

Kiongozi huyu anautanabaisha umma kuwa ndani ya chama chao kwa sasa suala la rushwa ndiyo jambo kubwa na ‘nambari wani’ ambalo linapewa kipaumbele.

Kipaumbele ninachozungumzia ni kwamba ni jambo ambalo linapiganiwa kulitokomeza kama si kulipunguza kuanzia ngazi zote, ingawa kwa uhalisia jitihada zinatia shaka kutokana na neno rushwa kugezwa na kuitwa takrima.

Kikohozi cha Mangula hakijitofautishi na ugonjwa wa kifua na mafua maana kikohozi cha mafua huenda sambamba na kifua yaani rushwa na takrima ni mapacha wa tumbo moja.

Hoja ya Mangula ya kutokomeza rushwa kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za chama hicho ni nzito na haipaswi kupita bila kuitazama kwa kina.

Kiongozi huyu anapaswa kutuambia kuwa CCM ya kwao (ya kina Nyerere, Mangula na wenzao wengine) hali ilikuwaje na sasa hali ikoje.

Ninaamini CCM inaongozwa na Katiba ambayo misingi ya uendeshaji wa chama imejaa humo ikiendelea kuogelea.

Kila ngazi ina mamlaka kamili ya kushughulikia masuala ya maadili, swali linabaki kuwa, kauli hizi za Mangula zinalenga ngazi gani mbona wenzake wa ngazi za chini hatuwasikii?

Je, wao pia ni wala rushwa na watoa rushwa? Lakini je, watawezaje kukemea rushwa wakati kila mmoja anakuwa na ‘bepari’ lake? Mfano mwenyekiti anakuwa na wagombea wake ambao wanamlisha pumba, vivyo hivyo katibu naye kwa kila ngazi anakuwa na jini lake je, hapo rushwa itaisha ndani ya CCM?

Wakati wakiangaliwa watoa rushwa je, wapiga kura wanaopewa wamekatazwa kuzipokea hizo rushwa au takrima kama zinavyopambwa? Jamii yetu ina maadili ya kukataa kununuliwa?

Tujiulize kama taifa nani katurithisha tabia hii ya kutoa rushwa na kupokea rushwa? Natamani wanaotaka kuwa viongozi wajitokeze na
kupelekwa JKT kwa ajili ya mafunzo ya uongozi na uzalendo, lakini napata shaka maana baadhi ya hawa hawa waliopitia huko ndiyo taabu kwelikweli.

Oktoba 14, mwaka huu nilimsikiliza na kukubaliana na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda, hasa pale aliposema kuwa mafunzo ya JKT ni
sawa na mafunzo ya kumfunda binti anayetaka kuolewa (Kitchen Party).
Aliyasema hayo alipohojiwa na kituo kimoja cha Redio jijini Dar es Salaam ambapo alifafanua kuwa mafunzo yale hayasaidii kwa sababu muda anaofundwa mhusika ni mchache kuliko muda ambao ataenda kuyaishi maisha halisi
na kupambana na changamoto zake.

Najiuliza kuwa leo hii mbali na CCM, ni kiongozi gani yupo madarakani kutoka kwenye chama chake chochote cha siasa hapa nchini ambaye hakutumia pesa kupata nafasi aliyonayo?

Macho yangu yanakosa nuru maana nawaona kwa mbali sana na kwa kutumia kurunzi.
Maandiko yanasema dhambi ya uzinzi haitoki kwa maombi bali kwa kukimbia kwa miguu ya mtu mwenyewe.

Hata dhambi ya rushwa naamini ndani ya CCM na Tanzania kwa ujumla haiwezi kutoka kwa matamko ya Mangula, bali kwa sisi sote kama taifa kuikataa kwa dhati ya mioyo yetu kisha tuseme vita tumepigana, mwendo tumeumaliza, imani tumeilinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles