Imechapishwa: Tue, Oct 10th, 2017

MAJERUHI YAITESA YANGA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wakiendelea kujiandaa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar unaotarajiwa kupigwa Jumamosi Uwanja wa Kaitaba, Kagera, wachezaji majeruhi ambao pia ni tegemeo wameendelea kuitesa timu hiyo.

Tangu ligi imeanza, mshambuliaji, Amissi Tambwe, hakucheza kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya goti na hivi karibuni Donald Ngoma naye ameiweka timu hiyo katika wakati mgumu baada ya kuumia nyama za paja, ikiwa ni pamoja na Thaban Kamusoko aliyeumia goti.

Pia kwenye mchezo wa juzi wa kirafiki dhidi ya timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) inayoshiriki Daraja la Kwanza (FDL), wachezaji hao hawakuwepo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi, ambapo mabingwa hao watetezi walishindwa kutamba baada ya kulazimisha suluhu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Timu hiyo inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi tisa, ikiwa sawa na Tanzania Prisons zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema baadhi ya wachezaji ambao ni kikosi cha kwanza ni majeruhi, lakini kikosi hicho kitakuwa sawa baada ya kufanyia kazi mapungufu yaliyopo.

“Wachezaji wengi waliocheza leo (juzi) walikuwa hawatumiki, hivyo leo tumeamua kuwapanga, vile vile baadhi ya nyota wetu wanaocheza kikosi cha kwanza ni majeruhi na wengine wameshaanza kuwa fiti lakini viwango vyao bado havijarudi ila baadaye naamini watabadilika na kutuletea matokeo,” alisema.

Alisema bado wanaendelea kuifanyia kazi safu ya ushambuliaji ambayo wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini tatizo linakuja kwenye umaliziaji ili lisijitokeze kwenye mchezo unaowakabili mbele yao.

Akizungumzia mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Nsajigwa alisema anaifahamu ni timu nzuri, lakini lazima wapambane kupata pointi tatu muhimu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Tunawaomba mashabiki wa Yanga wasikate tama, waendelee kutupa sapoti kwenye michezo yetu ili wachezaji wapate morali na kufanya vizuri zaidi,” alisema.

Upande wake daktari wa timu hiyo, Edward Bavu, alisema wachezaji ambao ni majeruhi, Ngoma na Kamusoko, wataanza kesho mazoezi mepesi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Nilikuwa sipo na timu lakini naendelea kufuatilia taarifa za wagonjwa hivyo kesho (leo), Ngoma na Kamusoko pamoja na Tambwe wataendelea na mazoezi mepesi ambayo yataendelea kesho kwenye Uwanja wa Uhuru,” alisema.

Timu hiyo inatarajia kuondoka Alhamisi kuelekea Kagera kwa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini humo.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

MAJERUHI YAITESA YANGA