27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Viwanda 4,000 vimejengwa chini ya Serikali ya awamu ya tano

Aveline Kitomary, Dar es salaam

WAZIRI Mkuu  Kassim Majaliwa amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa na hivyo kufanya sekta hiyo kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 8.05 na kutoa ajira 306,180 mwaka 2018. 

Akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli jana Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa tuzo za Rais kwa wazalishaji bora wa viwandani (PMAYA)  mwaka  2018 alisema  kutokana na sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa, Serikali itavipa kipaumbele viwanda vinavyotumia malighafi za ndani zaidi.

Tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) ilishirikisha makampuni 61 ambapo mshindi wa jumla ilikuwa ni kampuni ya Hanspaul iliyoko mkoani Arusha.

“Sekta ya viwanda imeendelea kuongeza pato la taifa na mwaka 2018 imeongezeka kwa asilimia 8.05  tofauti na mwaka  2017 ambao ilikuwa asilimia 7.67, Aidha, katika kipindi cha mwaka 2018 Sekta ya viwanda ilichangia asilimia 18.1 ya mauzo yote ya nje, ikilinganishwa na asilimia 15 mwaka 2017 pia, takwimu zinaonyesha kwamba katika mwaka 2018 Sekta ya viwanda imetoa ajira rasmi 306,180 ikilinganishwa na ajira 280,899 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 9.  

“Mkakati wetu wa kuendeleza viwanda nchini kipaumbele kimewekwa katika viwanda ambavyo vinatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini, tunahitaji kupunguza uuzaji wa mazao yetu ya kilimo, misitu, madini na maliasili nje ya nchi yetu yakiwa ghafi, hali kadhalika tunalenga kutumia rasilimali zilizopo nchini kuzalisha  bidhaa ambazo  hivi sasa tunaziagiza kutoka nje.

“Shabaha yetu ni kutosheleza mahitaji ya ndani ya bidhaa za viwandani, na kuwa na ziada tutakayouza nje  ya nchi ili kupata fedha za kigeni, kukuza ajira na kuongeza kipato cha Watanzania kwa ujumla,yote haya yatawezekana kama tutatengeneza miundombinu kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa bora,”alisema Majaliwa. 

Alisema ili kufikia lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa na uchumi wa viwanda Serikali haina budi kuhahakikisha ukuaji wa uchumi unafikia asilimia 12 kwa mwaka.

“Ikiwa ni mchango wa viwanda katika Pato la Taifa usiopungua asilimia 15,utoaji wa ajira rasmi na za moja kwa moja uongezeke na kufikia asilimia 40 ya ajira zote; na,pia ni muhimu sekta ya viwanda iweze kuiingizia nchi mapato ya fedha za kigeni zaidi ya asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni,”alieleza. 

Aidha alisema kuwa serikali inaendelea kutatua changamoto zinazoikumba na kurudisha sekta ya viwanda nchini kwa kushirikiana na sekta ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanya biashara. 

Aidha Waziri Majaliwa alimpongeza Subhash Patel kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CTI pamoja na wadhamini waliojitokeza kudhamini tuzo hizo.

“Kuchaguliwa kwako ni ishara tosha kwamba Wanachama wa CTI wanakupenda na wanatambua mchango wako mkubwa katika sekta ya viwanda pamoja na uwezo na uzoefu wako wa muda mrefu wa kusimamia masuala ya viwanda nchini,” alisema.

Kwa upande wake mshindi wa jumla wa tuzo hiyo Satbir Singh alitoa ushauri hasa kwa vijana ambao wanamalengo ya kuanzisha viwanda wawe na uthubutu.

“Kila kitu ni uthubutu na kutokukata tamaa ni muhimu kila mtu apambane kuhakikisha anafanikisha ndoto zake au malengo yake kwahiyo nawaambia hasa vijana wasikate tamaa katika wakati mgumu wa biashara wanaopitia kila kitu ni uvumilivu na uthubutu,”alisema Singh

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles