26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA: TUTAENDELEA KUNYANG’ANYA MASHAMBA

majaliwakassim

NA MWANDISHI WETU – ARUSHA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali itahakiki na kuwanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru na wanakijiji wa Kijiji cha Bwawani na Kitongoji cha Mapinu, Kata ya Nduruma akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

“Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini, na tangu alipokabidhiwa amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo?” alisema.

Alisema Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza..

“Nina taarifa kwamba hapa Arumeru kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na hawajayaendeleza. Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha kinyume na mikataba yao ya umiliki. Hatutawavumilia,” alisema.

Alisema Wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja mmoja, na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo.

“Kuanzia leo, marufuku Jeshi la Polisi kutumiwa na mtu binafsi kuwanyanyasa wananchi. Mtafanya hivyo kama kuna uvunjifu wa amani na si vinginevyo,” alisema.

Alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, anatarajia kwenda mkoani Arusha kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyarudisha serikalini.

Awali, akisoma taarifa ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti,  alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji, ambayo hayajaendelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles