28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Majaliwa: Tanzania ipo tayari kushirikiana na Afrika Kusini

Mwandishi wetu-Morogoro

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Afrika Kusini katika kutimiza azma yake ya kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.

Alisema hayo jana wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro.

Alisema Tanzania inahitaji uungwaji mkono na Serikali ya Afrika Kusini hususan katika kipindi hiki ambacho imedhamiria kuimarisha shughuli za uzalishaji kupitia viwanda kwa lengo la kufikia uchumi wa kati.

Akizungumzia kuhusu eneo la Mazimbu, Majaliwa alisema lina uhusiano na historia ya nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.

Alisema eneo la Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya vuguvugu la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

 “Tanzania ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele (Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.”

Alisema sera za ubaguzi wa rangi zilikoma Februari 1994 na kufuatiwa na uchaguzi huru na wa haki alipopatikana Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Nelson Mandela Mei 1994.

 “Tunapoongelea kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, siku zote tutawakumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mzee Nelson Mandela kwa utumishi wao uliotukuka kwa kujenga misingi imara ya umoja katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.”

Alisema misingi imara iliyojengwa na waasisi hao, imekuwa chachu ya ushirikiano kwenye majukwaa ya Kimataifa hususani katika kupambana na ubaguzi wa kiuchumi na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

Majaliwa alisema namna pekee ya kuwaenzi viongozi hao ni kuendelea kujenga umoja na kushirikiana katika kuimarisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa aliishukuru Tanzania kwa mchango iliyoutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.

Alisema Serikali yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali na kukuza teknolojia.

Pia amesema watasaidiana na SUA kuboresha miundombinu mbalimbali ili kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa.

“Tutaboresha na shule katika eneo hili na kuweka utaratibu wa walimu wake kutembeleana na wa Afrika Kusini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.”

Rais Ramaphosa aliwasili katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi na kupokelewa na Waziri Mkuu. Kisha alitembelea campus ya Solomon Mahlangu na kujionea maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakikutana na kupanga mipango mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles