25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA: SIJARIDHISHWA UJENZI KITUO CHA FORODHA SIRARI


Na MWANDISHI WETU-MARA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa kituo cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.

Kutokana na hali hiyo, amemtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), afike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma akiwa na mkandarasi aliyejenga kituo hicho.

Hayo aliyasema jana baada ya kumaliza kukagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.

“Serikali haiwezi kuvumilia ujenzi wa hovyo kiasi hiki, namtaka Kamishna wa TRA aje ofisini kwangu Januari 25, 2018 pamoja na mkandarasi aliyejenga kituo hiki akiwa na nyaraka zote za ujenzi wa jengo hilo,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango kwani kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.

Alishuhudia kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia sheria na wajiepushe na biashara za magendo.

Waziri Mkuu alisema magendo yanaikosesha Serikali mapato, hivyo bidhaa yoyote itakayokamatwa ikiingizwa nchini kwa njia za magendo, itataifishwa pamoja na chombo cha usafiri kilichotumika.

Mbali na hilo, pia ametembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Borega, ambako amewasisitiza wananchi wasimamie elimu ya watoto wa kike ili wafikie malengo yao.

Alisema Serikali imeweka sheria kali kwa yeyote atakayekatisha masomo kwa watoto wa kike iwe kwa kumpa ujauzito au kumuoa, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kamwe wasijihusishe katika mambo ambayo hayahusiani na masomo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles