31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA: KILA ALIYEKULA FEDHA ZA USHIRIKA ATAZILIPA

Na MWANDISHI WETU-LINDI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali haitahusika na ulipaji wa deni la fedha za Ushirika na badala yake kila aliyekula fedha hizo atazilipa mwenyewe.

Waziri Mkuu ameyasema hayo juzi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Liwale, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa wilaya.

Waziri Mkuu, ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi, amesema Serikali haiwezi kukubali Ushirika ukafa nchini kwa ajili ya watu wachache wasiokuwa waaminifu.

Alisema watu wote waliopewa dhamana ya kuongoza vyama vya ushirika na kuamua kujinufaisha kwa kula fedha za vyama watazilipa.

Kutokana na hali hiyo, Majaliwa amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kufanya ukaguzi katika vyama vyote vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili kubaini ni wakulima wangapi wanadai.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi na kubaini idadi ya wakulima wanaodai na kiasi cha fedha wawachukulie hatua wahusika wote kwa mujibu wa sheria.

Awali, Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, ambapo aliwataka watumishi wa umma nchini kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Lazima wananchi waone na wanufaike na kazi inayofanywa na Serikali yao, hivyo ni wajibu wa watumishi kuwatumikia wananchi popote walipo na si kukaa maofisini,” alisema Majaliwa.

Pamoja na hali hiyo, aliwataka watumishi hao kupanga mipango itakayoleta tija kwa wananchi na si vinginevyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles