23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa awapa somo viongozi wa dini

Mwandishi wetu-Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuimarisha malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana na kuepusha mmomonyoko wa maadili ili Taifa liendelee kung’ara, kuheshimika na kusifika.

Majaliwa alisema jana mjini Dodoma alipomuwakilisha Rais Dk John Magufuli kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ulioambatana na harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitegauchumi cha jumuiya hiyo.

Alisema Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo CCT katika kutengeneza mustakabali mwema na ustawi wa familia kupitia mahubiri ya injili na malezi ya kiroho kwa waumini.

 “Mtakubaliana nami kuwa siku zote Taifa imara msingi wake hujengwa na familia imara,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali inatambua mchango wa malezi ya kiroho katika ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla na mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga watumishi wa umma ambao wamelelewa katika misingi ya kumcha Mungu.   

Alisema Serikali inaamini watumishi wa namna hiyo watachapa kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu na kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma.

Akizungumzia kuhusu harambee hiyo ambayo jumla ya Sh. milioni 357.35 zilipatikana, alisema ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa CCT wa miaka mitano (2017 22) wenye lengo la kuiwezesha CCT kujitegemea kwa kuwa na vitega uchumi vyake ambavyo vitawawezesha kujiendesha kwa asilimia 80.

Aliipongeza CCT kwa kuanza kuchukua hatua za kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kiuchumi kwani zinahitajika nguvu za pamoja katika kuhakikisha wanawahudumia Watanzania na kuwaletea maendeleo.

“Kujizatiti kwa CCT katika kufikia malengo yake ya kujitegemea kiuchumi ni muhimu katika kutimiza kusudio na agizo la Mungu la kuwahudumia wahitaji ambao ni Watanzania lakini pia mtakuwa mnajaliza juhudi za Serikali katika wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.”

Alisema kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za CCT na madhehebu mengine ya dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta za elimu, maji, afya na shughuli za ujasiriamali.

Majaliwa alisema suala la kujitegemea ndiyo msingi wa uongozi wa Rais Magufuli wa kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025 na katika kufanikisha hilo, Serikali imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi.

Alisema kiwango cha utegemezi kutoka kwa Washirika wa Maendeleo katika bajeti, kimepungua kutoka asilimia 12.5 mwaka 2017/18 hadi asilimia nane 2019/20.

“Kuimarika huko kwa bajeti yetu kunakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kupungua kwa umaskini wa mahitaji muhimu,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Matonya, alisema jumuiya hiyo imeanzisha mkakati wa kuwa na vitegauchumu vyake kwa lengo ni kuondokana na utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles