27.6 C
Dar es Salaam
Saturday, March 30, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa awajibu ACT ukaguzi wa miradi Z’bar

Ramadhan Hassan – Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ataendelea kutoa maagizo mahali popote nchini kwa kuwa yeye ndiye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba alichofanya visiwani Zanzibar ni sahihi.

Hatua hiyo imekuja baada ya Chama cha ACT Wazalendo upande wa Zanzibar kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Nassor Mazrui, kupinga agizo alilolitoa Waziri Mkuu wiki iliyopita katika ziara yake visiwani humo wakati akikagua miradi ya maendeleo.

Alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hana mamlaka ya kuingilia na kutoa maagizo Zanzibar kwa mambo ya yasiyo ya Muungano kwa mujibu wa  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambapo alidai zimeainisha waziwazi mamlaka ya Serikali mbili zilizopo.

Hata hivyo jana Majaliwa alitoa alijibu mapigo hayo jijini Dodoma, wakati akifunga semina ya ushiriki wa vyombo vya dola katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini, ambayo ilihudhuriwa na makamanda wa polisi wa mikoa, wakuu wa vyombo vya usalama, wapelelezi wa mikoa pamoja na watendaji wa Wizara ya Madini.

Waziri Mkuu alisema yeye ndiyo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo anapaswa kutoa maagizo mahali popote pale Tanzania Bara au Tanzania Visiwani

“Nimekuja kufunga kikao hichi cha kazi, nitumie fursa kutoa maagizo mbalimbali ndiyo utaratibu wetu lazima tuelezane, lazima tuambizane ili tuweze kufanya kazi vizuri.

“Nakumbuka nilifanya ziara hivi karibuni visiwani, nilikagua miradi na niliona kazi nzuri inafanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nilipokuja kutoa maagizo ikaonekana sipaswi kutoa maagizo mimi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Napaswa kwenda mikoa yote nchini kuona shughuli za miradi zinavyotelezwa lakini mimi pia ndiyo mtendaji mkuu na nimepewa jukumu la kusimamia ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho kipo katika pande mbili.

“Nipo tayari kutoa taarifa kwenye mkutano mkuu na kwa hiyo nikifika katika mradi nitauona, nitapongeza, nitasikia lakini pale panapokuwa na ubovu nitaeleza, siwezi kuwa naenda nasifia tu hata vile ambavyo vibovu halafu nikarudi nitakuwa sijawatendea haki Watanzania.

“Kwa hiyo nilichokifanya ni sahihi na hasa maeneo ambayo watanzania wanapata tija na Tanzania ni Bara na Visiwani. Na nyie mnapopita huko angalieni  haya ambayo yanafanywa na yote yawe na tija kwa watanzania pale ambapo panahitaji marekebisho waambieni,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu hao wa vyombo vya dola kuhakikisha wanalinda rasilimali za nchi na kuhakikisha zinatumika vyema.   

“Ni wajibu wetu kwa pamoja katika nafasi tulizonazo kuhakikisha tunavutia wawekezaji wapya katika maeneo yetu. Hili la kuvutia wawekezaji hususani kwenye sekta ya madini linaweza kuongeza tija kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwa litasimamiwa vyema,” alisema.

Alisema  mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa ulikua kutoka asilimia 3.3 mwaka 2016/17 na kufikia asilimia 5.1 mwaka 2018/19. Sekta ya madini katika kipindi hicho imekua kwa asilimia 13.7 na kushika nafasi ya pili kiukuaji ikitanguliwa na Sekta ya Ujenzi.

“Chachu ya mafanikio haya ni ushirikiano mzuri ulipo baina ya wadau wa sekta hii ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa hatuibiwi rasilimali zetu.

Nitoe rai kwa wizara kuhakikisha kuwa ushirikiano huu unaimarishwa na hivyo, kuiwezesha sekta hii kuendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi pamoja na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla,” alisema.

Pia Waziri Mkuu aliwataka wakuu hao kuangalia malalamiko ya wawekezaji na wadau wa madini kukamatwa na kubughudhiwa bila sababu za msingi.

“Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo kufuata taratibu. Hivyo basi, tumieni sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini,” alisema

Vilevile, Waziri Mkuu alitaka suala la wauzaji wa madini wakiwa wanaenda kuuza madini yao kukamatwa linatakiwa kuangaliwa kwa umakini.

“Tumeanzisha masoko ya madini ikiwa ni sehemu ya mkakati mahsusi wa Serikali kupunguza utoroshwaji wa madini. Awali ilionekana kuwa utoroshaji mkubwa unafanyika kwa sababu ya kwenda kutafuta soko lakini sasa masoko yapo.

“Hata hivyo kuna changamoto nyingine imeanza kujitokeza ya kuwakamata wadau wakiwa na madini hata kama wanapeleka sokoni.

“Natoa maelekezo kuwa, kuanzia sasa  wadau wote wanaopatikana na madini tuwape utaratibu wa kuelekea sokoni kuuza badala ya kuwakamata wakiwa wanaenda sokoni.

“Ni wajibu wetu kusimamia na kudhibiti utoroshwaji wa madini na pia ni jukumu letu sisi kama vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha kuwa masoko haya pamoja na Wafanyabiashara ya madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata Sheria wanalindwa na kuepuka kamata kamata zisizo na tija,”alisema

Majaliwa alisema huu ni wakati muafaka sasa kuanza kujihoji iwapo fungamanisho la Sekta ya Madini na sekta nyinginezo za uchumi linajitosheleza.

“Je, nini kifanyike kuwezesha fungamanisho hili?. Katika hili naelekeza kuwa viongozi wote mliopo, andaeni watu wetu kuwa tayari kutoa huduma migodini au kufanya biashara na migodi husika ili kupunguza uwezekano wa migodi hiyo kutegemea huduma hizo kutoka nje ya nchi.

“Suala la Migodi hii kutegemea huduma kutoka nje ya Nchi lifikie ukomo kwa kuhakikisha kuwa, kila huduma inayohitajika migodini, inapatikana nchini,”alisema.

Pia alitaka masuala ya  changamoto ya ubora wa ajira, mishahara na stahiki katika kazi zinazofanana na suala la unyanyasaji wa wafanyakazi yanatakiwa kuangaliwa kwa umakini.

Kwa upande wake,Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema wanakabiliwa na changamoto za utoroshwaji wa madini pamoja na madini feki ambapo wamekuwa wakijitahidi kukabiliana nazo.

“Baada ya mafunzo haya tutakuwa na mafunzo katika mikoa yote lengo letu uelewa uende kila mahali juu ya kulinda rasilimali za nchi,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles