24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa atoa agizo zito kwa Takukuru

Mwandishi wetu -Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ukamilishe mapema uchunguzi dhidi ya madudu yaliyoibuliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na wizi uliofanywa na viongozi wa Amcos kwa wakulima wa ufuta na korosho ikiwamo Wilaya ya Ruangwa.

Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akizindua jengo la Takukuru Wilaya ya Ruangwa lililogharimu Sh milioni 142.

Alisema pamoja na Takukuru kuendelea na utekelezaji wa majukumu ya kila siku, ikamilishe mapema utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. John Magufuli aliyoyatoa kwao kwa nyakati tofauti.

Alisema ameshuhudia kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya kupitia uchunguzi na ufuatiliaji wa madai ya malipo ya wakulima wa zao la ufuta na korosho.

“Kamilisheni chunguzi hizi zote kwa wakati ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliopatikana na hatia.

“Serikali imetoa msukumo wa pekee katika kushughulikia vitendo vya rushwa na ufisadi. Msukumo huo umechangia kwa kiasi kikubwa, hususan katika kipindi hiki, utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati kwa ufanisi na kwa wakati,” alisema Majaliwa.

Alisema wananchi wanatakiwa wafahamu kwamba nchi yoyote ambayo rushwa imetamalaki siyo rahisi kuwa na uwezo wa kiuchumi utakaoiwezesha nchi hiyo kumudu kulipa madeni ya ndani na ya nje.

“Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania tunashuhudia jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyolipa madeni,” alisema Majaliwa.

Alisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, imekuwa ikijipambanua na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

“Hivyo, kitendo hicho cha kuendelea kulipa madeni ni ishara ya mafanikio ya Serikali katika jitihada zake za kuzuia na kupambana na rushwa nchini,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia kuhusu jengo alilolizindia, alisema ni muhimu sana kwa taasisi nyeti kama ya Takukuru kumiliki majengo yake yenyewe.

 Kuhusu hali ya majengo ya ofisi za Takukuru katika ngazi ya mikoa na hata wilaya, amemwagiza Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa alishughulikie suala hilo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema jengo hilo limejengwa kwa miezi saba.

“Hadi kufikia hatua hii ya uzinduzi, jengo hili limegharimu jumla ya Sh 142,857,142.86,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Akizungumzia kuhusu uchunguzi, kiongozi huyo alisema kwa kipindi cha mwaka 2019 Takukuru imefanya uchunguzi kwenye tuhuma kubwa ikiwamo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Magufuli aliyoyatoa Jumanne Oktoba 15, mwaka jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ruangwa.

 “Kupitia uchunguzi ule, tumebaini kwamba zaidi ya vyama 30 vya msingi vya ushirika (Amcos) vya mkoani Lindi viliwadhulumu wakulima wa zao la ufuta kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 1.23.

“Kupitia uchunguzi huo tuliwakamata na kuwahoji zaidi ya viongozi 300 wa Amcos zilizokuwa zinahusika katika dhuluma hii.

“Tulifanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 1.042. Fedha hizi zilikuwa ni mali ya wakulima wa ufuta ambao walidhulumiwa na viongozi wa vyama vya Amcos,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles