30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya ebola

Mwandishi wetu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa wa ebola ambao umeendelea kuwepo katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.

Majaliwa alisema hayo jana wakati akiahirisha Mkutano wa 15 wa Bunge la Bajeti jijini Dodoma.

Alisema kutokana na mwingiliano wa nchi hizo, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana tishio la ugonjwa huo.

“Ugonjwa huu wa ebola umeendelea kuwepo Congo, umelipuka tena Uganda sote tunatambua upo mwingiliano wa nchi hizi, katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti.

“Lakini pia nitoe wito kwa Watanzania kuchukua hatua kutokana na hatari iliyopo katika ugonjwa huu,”alisema.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa dengue, Majaliwa alisema Janauri hadi Juni zaidi ya watu 4,282 waliathiriwa na ugonjwa huo na wanne walipoteza maisha.

Alitaja mikoa ambayo inaongoza kwa idadi ya wagonjwa wa dengue ni pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Singida, Pwani na Kilimanjaro.

Aidha, Majaliwa aliwataka wabunge kushiriki kwa wingi katika mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini kwa Afrika (SADC), utakaofanyika nchini Agosti.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba, aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha na kupiga kura.

Kuhusu Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint),  Majaliwa alisema kuanzia Julai Mosi Serikali itaanza kuutekeleza kwa lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara.

Alisema wakati kazi hiyo inaendelea Serikali itafanya ufutialiaji kuhusu utekelezaji wa mpango huo na kutathmini kama lengo limefikiwa.

“Utekelezaji wa mpango huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini, unaojidhihirisha kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo imefuta tozo kwamishi 54 zilizobainishwa kwenye mpango huo.”

Waziri Mkuu ametaja tozo zilizoondolewa au kupunguzwa ni pamoja na zinazosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Maji

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta tija, ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu kusambaza blueprint pamoja na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa wizara zote kwa ajili ya kusimamia utekelezaji katika maeneo yao.

Amesema kupitia mpango wa bajeti ya 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara kwa kutoa unafuu katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na shughuli nyingine jumuishi.

Wakati huohuo,Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na kilimo tegemezi cha mvua hususani kwenye zama hizi za mabadiliko ya tabia nchi, Serikali kwa sasa inaboresha kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuwatoa wananchi katika kilimo hicho.

Amesema hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni pamoja na kuunda upya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo inalenga kuiwezesha tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za umwagiliaji. Pia Serikali imehamishia tume hiyo Wizara ya Kilimo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza kilimo nchini.

”Ili tuweze kufikia lengo la kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2025, tayari nimeielekeza Wizara ya Kilimo isimamia kwa karibu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi.”

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Kilimo inatakiwa ihakikishe inasimamia vema miradi 22 ya umwagiliaji inayoendelea sasa pamoja na miradi mipya minane itakayojengwa nchini katika pindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles