30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataka viongozi wa dini kukemea unyanyapaa kwa wenye VVU

Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa viongozi wa dini kuelimisha waumini katika kukemea unyanyapaa kwa watu wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Rai hiyo aliitoa juzi jijini hapa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kushirikisha viongozi wa dini kupinga unyanyapaa kwa watu waishio na virusi vya Ukimwi pamoja na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Katika mkutano huo, viongozi waandamizi wa madhehebu yote ya dini walihudhuria ambapo kwa pamoja walisaini makubaliano ya kupinga unyanyapaa ikiwa ni pamoja na kupaza sauti kuhusu unyanyapaa kwa watu wanaoishi VVU.

Majaliwa alisema bado unyanyapaa ni mkubwa katika jamii, hivyo viongozi wa dini wanatakiwa kupaza sauti ili kuutokomeza.

Majaliwa pia alipiga marufuku matumizi ya neno waathirika wa Ukimwi na badala yake watumie neno maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Pia, amewataka wanaume kujitokeza kwa wingi kupima virusi vya Ukimwi na kuacha kutegemea vipimo vya wake zao.

“Wanaume mpo? Wito wangu tujitokeze kupima kwa wingi, baada ya tukio hili tuzunguke hapa nyuma tupime,” alisema Majaliwa.

Naye, Spika Job Ndugai alisema unyanyapaa upo hadi bungeni kwani alikutana na changamoto ya baadhi ya wajumbe aliowachagua katika Kamati ya Ukimwi kukakataa, hivyo akateua watu wengine.

Alisema mara baada ya kamati ya mwanzo kukataa, alitoa machozi, lakini alijipa moyo na kuteua nyingine ambayo imefanya kazi vizuri.

“Nilitoa machozi, unyanyapaa upo hadi bungeni, ilibidi niivunje kamati ile ya mwanzo na kuteua nyingine, hawa wamefanya kazi nzuri sana na naomba niwapongeze sana,” alisema Spika Ndugai.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato  Tanzania, Mchungaji Mark Malekana alisema kwa niaba ya Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania, watatumia makongamano ya vijana, wanawake, ibada na vyombo mbalimbali vya kanisa katika kuelimisha jamii kuhusu kutokomeza unyanyapaa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Deogratius Rutatwa, alisema kuna haja ya jamii kukaa kwa pamoja na kujadiliana jinsi ya kushikamana katika kutokomeza unyanyapaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles