26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataka kasi iongezeke ujenzi ofisi Wizara ya Fedha

FARIDA RAMADHANI Na PETER HAULE- DODOMA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza mkandarasi anayesimamia ujenzi wa ofisi mpya ya Wizara ya Fedha na Mipango ambaye anatoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha anaongeza rasilimali watu ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na ubora unaotakiwa.


Majaliwa alitoa agizo hilo jana, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi mbalimbali za wizara katika mji wa Serikali eneo la Ihumwa jijini Dodoma.


Alisema zimebaki siku 21 pekee kukamilisha ujenzi huo na lengo la Serikali ni kuona kazi hiyo imekamilika ifikapo Januari 31, mwaka huu.
Kwa muktadha huo, Majaliwa alionyesha hofu iwapo ujenzi utakamilika kwa wakati kutokana na kutoridhishwa na nguvu kazi iliyopo.


“Mimi ninapokuta watu wachache huku kukiwa na kazi zisizohitaji kusubiri siku mbili kama kazi ya kuweka bimu, natarajia kuona watu wangekuwa wanaendelea kufanya kazi hizo,” alisema.


Aidha, alisema ni wajibu wa mawaziri kutembelea ujenzi huo unaoendelea na kuona ubora wa jengo, aliongeza kwamba ni jukumu lao na wana uwezo wa kuonesha kuridhika au kutoridhika na ujenzi huo.


Majaliwa aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu kuhakikisha mazingira ya eneo la wizara linapandwa miti kulingana na ramani ya majengo ya muda na yakudumu.
Alisema kama watumishi waliopo ni wachache mkandarasi aongeze vijana ili ujenzi ukamilike mapema.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, aliahidi kusimamia maagizo ya Waziri Mkuu na kuhakikisha jengo linakamilika kwa wakati kwa kuwa hadi sasa asilimia 95 ya vifaa vyote muhimu vya ujenzi vimenunuliwa.


Akizungumzia suala la kuongeza nguvu kazi, Dk. Kijaji, alisema wizara itahakikisha mkandarasi anaongeza nguvu kazi kwa haraka kutoka mtaani au Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili ifikapo Januari 31, Wizara ikabidhiwe jengo rasmi.


Dk. Kijaji alieleza kuwa wizara ipo tayari kuhamia katika jengo hilo Februari mosi mwaka huu.


Naye mhandisi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Elisante Olomi, anayesimamia ujenzi wa ofisi za wizara hiyo, alisema ujenzi unaendelea vizuri na mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 75, huku akiahidi kuongeza mafundi wa kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles