28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ASIKITISHWA ONGEZEKO MIGOGORO YA ARDHI

Na SHOMARI BINDA – TARIME

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesikitishwa na ongezeko kubwa la migogoro ya ardhi, wakati Serikali imeweka wataalamu na kuwapa vitendea kazi vya kuwezesha kuitatua.

Kwa sababu hiyo, amewaagiza wakuu wa wilaya kuwashughulikia maofisa ardhi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiingiza wananchi kwenye migogoro kwa kutanguliza mbele masilahi yao.

Pia Majaliwa ametaka kila halmashauri kuwa na matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kupima viwanja kisha kutoa hati kwa kila mwananchi aliyepimiwa ili kuepuka migogoro kama hiyo.

Majaliwa alitoa maagizo hayo juzi mjini Tarime mkoani Mara wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya na Mji wa Tarime akiwa katika ziara ya kikazi.

Mbali na hayo, Majaliwa pia alisitisha uamuzi wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika eneo la Nyamwaga baada ya kubaini kuwa kujengwa katika eneo hilo kunaweza kuisababishia halmashauri kutumia fedha nyingi kulipa fidia wananchi wa eneo hilo.

Alisema mbali na fedha nyingi zinazoweza kutumika kwa ajili ya fidia ya eneo hilo, lakini pia uteuzi wake haukufuata taratibu na kushindwa kuzingatia jiografia ya halmashauri hiyo katika kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao.

Alisema baada kufanya uamuzi huo, Serikali itatuma wataalamu ili kuangalia maeneo hayo kisha kutoa ushauri kwa eneo linalostahili kujengwa makao makuu hayo.

Majaliwa alisema tayari zimeshakuwepo taarifa za kuibuka kwa migogoro ya wapi pa kujengwa makao makuu na Serikali haiwezi kukubali kuona hilo linatokea na kutaka taratibu zizingatiwe yanapofanyika masuala muhimu ya kuihudumia jamii.

Uamuzi huo ameufanya kama alivyofanya hivi karibuni wilayani Mbinga.

“Naagiza kusitishwa kwa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na wataalamu watakuja hapa hili kulifanya jambo hili kwa utaratibu unaofaa,” alisema Majaliwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Esther Matiko (Tarime Mjini) wote wa Chadema na Agnes Marwa (Viti Maalumu – CCM), wameshukuru ziara ya Waziri Mkuu kwa kuwa imesaidia kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles