25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Asasi zinazotoa elimu kwa wapigakura zisisemee chama chochote

Safina Sarwatt-Kilimanjaro

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amezionya asasi za kiraia zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa wananchi juu ya uboreshaji wa daftari la wapigakura, kutojihusisha na mijadala ya kisiasa wala ushabiki badala yake wafuate miongozo waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Daftari la Kudumu la Wapigakura katika viwanja vya Mandela, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema asasi hizo zinatakiwa kuwaelekeza wananchi umuhimu wa kujiandikisha, kupiga kura na kuwachangua viongozi wanaowataka wenyewe bila kushawishiwa.

“Msikisemee chama chochote cha kisiasa, waelekezeni wananchi umuhimu wa kujiandikisha, kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka wenyewe na siyo kuwashawishi ili wampigie kiongozi mnayemtaka.

 “Tume imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya asasi za kiraia. Rai yangu kwa asasi zilizopata vibali hivyo, ni kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.

Majaliwa alisema ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba.

Katika hatua nyingine, aliwahimiza vijana waliotimiza miaka 18 wajitokeze kujiandikisha.

 “Nitoe rai kwa vijana wote wa Kitanzania waliotimiza miaka 18 au ambao watatimiza umri huo ifikapo Oktoba 2020, wajitokeze kwa wingi na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

“Hawa ndio walengwa wakuu kwa sababu wanaingia kwa mara ya kwanza katika uchaguzi.

 “Ikumbukwe bila kujiandikisha hawataweza kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Kujiandikisha kutawahakikishia ushiriki katika uchaguzi,” alisema Majaliwa.

Alisema uandikishaji huo wa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, utafanyika nchi nzima na utakamilika Machi 2020.

 “Watakaohusika awamu hii ni wapigakura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale watakaotimiza miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama kata au jimbo na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao, mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa sambamba na kuwaondoa wapigakura waliopoteza sifa kama vile kufariki,” alisema.

 Katika hatua nyingine, Majaliwa aliziasa asasi za kiraia ambazo zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura, kujiepusha na ushabiki wa kisiasa.

“Tume imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya asasi za kiraia.

“Rai yangu kwa asasi zilizopata vibali hivyo, ni kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.

Alisema ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba.

 Mapema akitoa maelezo kuhusu uboreshaji huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage, alisema tume itaendelea kutumia teknolojia ya kielektroniki ya Biometric (BVR) na imeandaa BVR kits 3,000.

Alisema kwa Tanzania Bara, tume hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji kutoka 36,549 vilivyotumika mwaka 2015 hadi kufikia 37,407; kutokana na uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapigakura uliofanyika mwaka jana.

 “Kutokana na hilo, vituo 6,208 vilibadilishwa majina, vituo 817 vimehamishwa kutoka mtaa mmoja au kijiji kimoja na kwenda kingine na vituo 19 vilihamishwa kutoka kata moja kwenda kata nyingine.

“Kwa upande wa Zanzibar, vituo vya uandikishaji vimeongezeka kutoka 380 na kufikia 407. Kwa sasa kila kijiji au mtaa utakuwa na kituo kimoja,” alisema.

Alisema vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni na uboreshaji utafanyika kwa siku saba kwa kila kituo cha kujiandikisha, iwe ni Tanzania Bara au Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles