23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AMUWEKA KIKAANGONI MKURUGENZI

Na MWANDISHI WETU – SIKONGE

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya Sikonge, Evans Shemdoe, ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya ndani.

Alitoa agizo hilo jana alipozungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo  mjini Sikonge.

“Nataka maelezo yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya halmashauri, ambacho ni kiwango cha chini.

“Nzega TC wamefikisha asilimia 112, Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana asilimia 80, ni kwa nini wewe umeshindwa kufikisha kiwango hicho?

“Ninataka nipate maelezo pia ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato kwa maeneo mliyoshindwa kufanya vizuri na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa fedha. Niyapate maelezo hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” alisema.

Alipopewa nafasi ya kujieleza, Shemdoe alisema wamefikisha asilimia 76.7 na wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua   msimu uliopita.

Alisema hali hiyo ilichangia kushuka  mavuno ya   tumbaku miongoni mwa wakulima.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo washirikiane na watendaji na madiwani   kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia watendaji wa kata peke yao.

Juzi baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka halmashauri tano kati ya nane za mkoa huo, zitoe maelezo ni kwa nini zimeshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo kama   walivyoagizwa na Serikali.

“Halmashauri zilizovuka malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega DC. Nataka taarifa za halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni kwa nini hawajafikia malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni asilimia 80,” alisema.

  Waziri Mkuu pia aliutaka uongozi wa Mkoa wa Tabora uhakikishe wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wilaya hiyo   waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya mapato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles