31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa akerwa mimba kwa wanafunzi

Mwandishi wetu-Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kuwapo idadi kubwa ya mimba kwa watoto wa kike wilayani Ruangwa ni jambo linalomkera sana.

Alisema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Liuguru, Kata ya Narungombe wilayani Ruangwa juzi mara baada ya kukagua Shule ya Sekondari Liuguru.

Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ruangwa alisema njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kufanya shule za Sekondari Mnacho na Liuguru ziwe za bweni kwa wasichana pekee.

Alisema kuwa amechagua shule hizo ziwe za bweni kwa wanafunzi wa kike kama njia ya kuwaongezea fursa za masomo katika wilaya hiyo.

Majaliwa alisema kuwa amekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuona Shule ya Sekondari Liuguru inabadilishwa na kuwa shule ya bweni kwa wasichana pekee.

“Ndoto yangu ni kuona shule hii inakuwa ya wasichana peke yao. Na tukifanikiwa tutatengeneza kinamama wasomi, wanaojitambua, wenye maadili mema na wachapakazi.

 “Leo nimekuja kuwaeleza ndoto yangu. Tunahitaji kuona kila mtoto anayeenda shule anakuwa na uhakika wa kumaliza masomo yake ya elimu ya juu.

“Wilaya hii tuna shida ya idadi kubwa ya mimba kwa watoto wa kike, na mimi hili jambo linanikera sana.

“Tulikubaliana tuwe na kaulimbiu yetu kwamba ‘Ruangwa kwa maendeleo inawezekana’, lakini kwenye elimu tumekwama kuleta maendeleo kwa sababu dada zetu hawamalizi shule na sisi ndio wasababishaji,” alisema.

 Majaliwa alisema imewekwa sheria ya kuwafunga watu wanaowapa mimba wanafunzi, lakini bado haisaidii.

 “Njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kufanya shule hizi ziwe za bweni ili wakae hapa shuleni, wafundishwe bila kupoteza muda wa kwenda nyumbani au kukutana na vikwazo wawapo njiani kuja shule au kurejea nyumbani.

 “Kwa wenzetu kwenye mikoa mingine, mtoto wa kike akianza shule ya awali, atamaliza ya msingi, ataenda sekondari hadi chuo kikuu. Akimaliza kusoma, anarudi nyumbani kuja kufanya kazi kwao na kuwasaidia wengine waliokosa fursa.

 “Tunahitaji mabweni kwa ajili ya watoto wetu wa kike kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, tunahitaji nyumba za walimu ili wakae hapa na kuwalea wanafunzi wetu.

“Yakikamilika, tutawahamisha wavulana wanaosoma hapa na kuwapeleka shule za jirani au za bweni, ili hapa tuwaachie wasichana peke yao,” alisema Majaliwa.

Alisema kwa kuanzia zitatumwa Sh milioni 100 zitumike kujenga nyumba nne za walimu, kisha atatafuta fedha nyingine za ujenzi wa mabweni, bwalo la chakula, jiko na mahitaji mengine kadiri zitakavyopatikana.

Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wahakikishe wanakazania masomo kwani hakuna muujiza wa kufaulu mitihani kama hawatasoma kwa bidii.

“Wanangu wa ‘Form 2’ na ‘Form 4’ hakuna muujiza wa kufaulu mitihani iliyo mbele yenu. Ni lazima msome kwa bidii. Na msikubali kuishia ‘Form 4’, lazima mwende ‘Form 6’ na mkimaliza hakikisheni mnafika chuo kikuu,” alisisitiza.

Mapema, Mkuu wa shule hiyo, Samuel Diwani, alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007, hivi sasa ina walimu 11 ambao watatu kati yao wanafundisha masomo ya sayansi na wanane waliobakia wanafundisha masomo ya lugha na sanaa.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 109 ambao 51 kati yao ni wavulana na 59 ni wasichana, inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa nyumba tisa za walimu, ukosefu wa maabara mbili na iliyopo moja haijakamilika kwa asilimia 100.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles