23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAHIGA AMSHAURI JPM KUIMARISHA USALAMA

Na GABRIEL MUSHI-DAR ES SALAAM           |        


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, amemshauri Rais Dk. John Magufuli kutafuta mikakati ya kuimarisha usalama pindi anapopambana na walarushwa na wabadhirifu wa rasilimali za Tanzania.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi katika maadhimisho ya 55 ya Siku ya Afrika na kukutanisha mabalozi wa nchi mbalimbali waliosherehekea na kutafakari mbinu za kulikomboa Bara la Afrika katika ubeberu.

Mahiga alisema kutokana na mapambano aliyoyaanzisha Magufuli dhidi ya rushwa, ufisadi, ujangili wa pembe za ndovu na mitandao ya dawa za kulevya, ni dhahiri ametengeneza maadui wengi.

“Sasa anapopambana na hawa anatengeneza maadui ambao lazima atafute mkakati wa kuimarisha usalama, huku anapambana nao,” alisema.

Mahiga alisema mapambano hayo aliyoyaanzisha ni ya kipekee kwa sababu yamewahi kuzipa tabu nchi mashuhuri kama Marekani.

Pia alisema katika ripoti iliyoandaliwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, imebainisha fedha zinazotoroshwa Afrika kwenda nje ni zaidi ya theluthi moja ya utajiri wa bara hilo.

“Nimewakumbusha watu kuwa Rais Magufuli ametangaza kuwa pamoja na umoja wetu, kuna vitu ambavyo bado ni changamoto katika kujenga uchumi wetu, kwa mfano rushwa na ufisadi.

“Hivyo fedha hizo zinatoroshwa Afrika na watu wetu humu ndani kwa sababu ya rushwa na ufisadi ambao sasa Rais Magufuli anapambana nao,” alisema.

Mahiga alisema pamoja na kukumbuka viongozi waliopigania umoja na ukombozi wa nchi za Afrika, ni vyema pia kuikumbuka jamii ya watu wa kawaida walioongoza mapambano na maandamano katika kulikomboa bara hili.

“Katika uhuru hatungekuwa na mawazo na busara kama ya ya Mfalme Solomon, kama huna watu nyuma yako, huwezi kuwa na mafanikio katika kupata uhuru. Katika ujenzi wa uchumi hata ukiwa na akili kama Einstein, ukiwa peke yako huwezi kujenga uchumi, lazima uwapange watu ili mikakati hiyo iwanufaishe.

“Hivyo tunapokumbuka viongozi waliotoka huko nyuma na walipopo sasa, pia tukumbuke jitihada za watu ambao walipigana au kuandamana kupata uhuru. Na watu ambao sasa lazima tuwapange kupata uhuru wa uchumi,” alisema.

Pia alisema mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Mauritania, utakuwa na kaulimbiu ya jinsi ya kupambana na rushwa katika Afrika.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema Watanzania na Waafrika kwa pamoja wanatakiwa kutumia umoja uliopo kuongea kwa sauti moja katika kudai haki ya kibiashara kutoka kwa nchi zilizoendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles