33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yazuia mwili wa marehemu kuzikwa

NA MWANDISHI WETU

MAHAKAMA  ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, imezuia mwili wa mfanyabiashara maarufu wa madini wa Arusha, Jubilate Benjamin Ulomndugu, kuzikwa mpaka  kifo chake kitakapochunguzwa kwa kina na maofisa wa Jeshi la Polisi na madaktari.

Ndugu wa karibu wa marehemu wanapinga anayedaiwa kuwa mke wa marehemu, Zainabu Rashid, kufanya mazishi ya mumewe kwa madai kuwa hakuwa mke halali wa ndoa.

Hata hivyo, mahakama hiyo mbele ya Hakimu Devotha Msofe imezuia ndugu wa marehemu kufanya chochote kuhusiana na mali za marehemu hadi shauri mama litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Jubilate alifariki dunia Januari 15, 2019 katika Hospitali ya Aga Khan   Nairobi, Kenya na baadaye kuhamishiwa Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa huduma ya mazishi   lakini maziko yake hayakuweza kufanyika baada ya mke huyo kupeleka mgogoro huo mahakamani baada ya ushauri uliotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Hai.

Katika hati yake kinzani ya kupinga kesi iliyopo mahakamani, mmoja wa ndugu zake   marehemu, Onesy Benjamin Ulomi, amekanusha   kuwa Zainabu Rashid, ambaye ndiye mwombaji katika shauri hilo, kuwa mke wa  sheria wa marehemu na amemtaka athibitishe ukweli huo.

“Jubilate Benjamin Ulomi alikuwa mdogo wangu na hakuwa na kwa uelewa wangu hakuwahi kufunga ndoa ya sheria na mwombaji,” anadai Onesy, ambaye ni miongoni mwa walalamikiwa wanne katika shaurio hilo.

Hayo anayaeleza katika kiapo chake kilichowasilishwa mahakamani na wakili wake,  Joseph Ngiloi kutoka kampuni ya uwakili wa Makoa Attoneys.

Walalamikiwa wengine katika mgogoro huo ni Werandumi Benjamin Ulomi, Awadi Ulomi na Abdulrasul Ulomi.

Anadai  Jubilate ambaye alikuwa ametengana na kanisa lake kwa kuwa na watoto wengi na wanawake tofauti bila kufuata mwongozo wake wa roho, aliungana tena katika kanisa lake baada ya toba mbele ya Mchungaji Chambulila wa Kaniasa la Msamaria Mwema (Good Samaritan) na akasema kuwa hakuwahi kuwa na ndoa yoyote iliyosajiliwa.

Onesy amedai   baada ya kupitia maombi yaliyopo mahakamani amebaini   maombi yaliyoletwa hayana mashiko yoyote kwa vile hayajaungwa mkono na maombi yoyote ya awali ambayo yanaweza kuangaza ushahidi wa masuala ya msingi  kuthibitisha amri   zitakazolewa   kesi mama itakaposikilizwa.

Baada ya kutoa zuio hilo, Mahakama   iliamuru shauri hilo litajwe  Februari 7 mwaka huu. Katika hati yake ya kuunga mkono maombi yake, mwombaji anasema   alikuwa mke halali na wa  sheria wa Jubilate na waliishi   pamoja kama mume na mke kwa miaka 12.

Anadai   walibarikiwa kuwa na watoto wawili na walitengana kwa muda isivyo halali, lakini alibakia kuwa mke wa  sheria wa marehemu hadi tarehe ya kufa kwake. Mwombaji ameeleza kuwa   baada ya kufariki dunia mume wake, Januari 18, 2019, pande zote mbili zilikutana  kukubaliana juu ya njia bora za mazishi.

Mwombaji anadai hata  Januari 19, 2019, kila kitu kilibadilishwa na walalamikiwa pamoja na ndugu zake wengine wa ukoo na kuzuia mwili wa marehemu kuchukuliwa Merelani kama moja ya mila yao, kitendo ambacho kilimwongeza shaka   juu ya nini kilichokuwa chanzo ya tatizo hilo.

Anadai Onesy alitoa maelekezo kwa watumishi wa sehemu ya kuhifadhia miili ya marehemu kwamba hakuna mtu anayepaswa kuruhusiwa kuona mwili huo, hali ambayo ilimlazimisha kuandika barua kwa Mkuu wa Wilaya kuomba msaada wake.

Hata hivyo,   Mkuu wa Wilaya alimshauri kutafuta taratibu za  mahakama kwa kuwa ofisi yake haikuwa na mamlaka ya kutatua suala hilo.

Hapo ndipo  mwombaji alipoamua kukimbilia mahakamani kutafuta haki zake juu ya mgogoro huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles