30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yawaonya kina Mdee

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapa onyo kali Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wenzake watatu na imewahurumia kuwafutia dhamana.

Uamuzi ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kupitia hoja za pande zote kuhusu kwanini washtakiwa wasifutiwe dhamana.

“Hakuna ubishi kwamba Novemba 15 washtakiwa wanne hawakuwepo mahakamani na wenzao watano walikuwepo, hoja kwamba wamezoea kesi inaingia saa nne ni dhana yao tu.

“Najiuliza kwanini wengine watano walikuja mahakamani na wadhamini wao na wengine wanne na wadhamini hawakufika, kuna tatizo, mlifanya makusudi.

“Haya maelezo mliyotoa hayashibiki, mawazo yangu ni kwamba pamoja na tatizo lililopo, hatua ya kuwafutia dhamana ni hatua kali sana.

“Mnapewa onyo kali, msirudie tena, maelezo yenu hayaingii akilini, nachukulia mlifanya makusudi na kwenda kujisalimisha polisi ni kuogopa kitu ambacho kingewatokea, dhamana zenu zitaendelea,” alisema hakimu Simba.

Alisema kwa upande wa Mchungaji Peter Msigwa kwamba mdhamini wake mmoja kahama chama, mahakama inamtaka atafute mdhamini mwingine ama amlete mdhamini aliyehama chama ajieleze kama anaendelea kumdhamini.

“Take care, tofautisheni vitu vingine na masuala ya mahakama,” alisema hakimu Simba na kumwamuru mshtakiwa John Heche kufika na wadhamini wake mahakamani kati ya Novemba 26 na 29.

Wabunge hao wanne waliolala Segerea ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Heche, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa, Mbunge wa Kawe, Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Jana washtakiwa wote walikuwepo mahakamani isipokuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye anadaiwa kulazwa chumba namba 507 katika Hospitali ya Aga Khan.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai, ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam Bulaya alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili; Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara mshtakiwa Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki akitamka matamshi kwamba; “kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii… wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano… watu wanapotea… watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome…”

Kwamba maneno hayo yanadaiwa yalielekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles