24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAOMBA IFUTE KESI YA MALINZI

PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA

UPANDE wa utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuifuta kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wawili, kwa sababu upelelezi wa kesi hiyo unachelewa.

Wakili wa utetezi, Abraham Senguji, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Alidai inaonekana upelelezi unachelewa kwa madai kuwa, kinachosubiriwa ni kupata jalada kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hivyo basi mahakama hiyo inaweza kuwaachia wateja wake chini ya kifungu cha 225 wakati upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.

Alidai mpaka sasa wateja wao wanaendelea kuumia kwa sababu makosa yanayowakabili hayana dhamana.

Alidai kutokana na hali hiyo, mahakama hiyo inaweza kuiondoa kesi hiyo chini ya kifungu kingine cha 91(1), ili upande wa Jamhuri uweze kukamilisha upelelezi na kwamba watakapomaliza wanaweza kuwakamata tena.

Hata hivyo, Wakili wa Jamhuri, Leonard Swai, alidai kuwa, wanaendelea kufuatilia jalada la kesi hiyo kwa DPP.

Alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba jalada lilikwenda kwa DPP ili aweze kulipitia na kwamba akimaliza atawapa maelekezo.

Alidai kuwa, hakutakuwa na maslahi kwa washtakiwa hao kuachiwa na kukamatwa tena kwa sababu wakiletwa mahakamani watasomewa upya mashtaka yao.

Aliiomba mahakama hiyo kuwapa muda ili waweze kukamilisha.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, alisema upande wa Jamhuri na utetezi ushirikiane kufuatilia kwa DPP ili waweze kujua upelelezi ulipofikia na kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na aliyekuwa mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga, ambao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashtaka 28, likiwamo la utakatishaji fedha wa Dola za Marekani 375,418.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles