28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAMZUIA BEMBA KUGOMBEA URAIS DRC

KINSHASHA, DRC

MAHAKAMA ya Juu ya Katiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imemwondoa rasmi kiongozi wa upinzani, Jean-Pierre Bemba aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kumrithi Rais Joseph Kabila katika kinyangayiro cha urais.

Katika uamuzi uliotangazwa kwenye televisheni ya taifa juzi jioni, mahakama ilisema Tume ya Uchaguzi ilikuwa sahihi kumwondoa Bemba kutoka orodha ya wagombea urais wenye sifa kutokana na kukutwa na hatia ya kuhonga mashahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Mahakama hiyo ilisema kuhonga mashahidi ili kuhujumu kesi iliyokuwa ikimkabili ni aina ya rushwa, ambayo imekatazwa katika sheria za uchaguzi za DRC.

Tume ya Uchaguzi ilikuwa imemwondoa Bemba na wagombea wengine sita wakiwamo mawaziri wakuu watatu wa zamani Adolphe Muzito, Antoine Gizenga na Samy Badibanga katika orodha ya wagombea waliopitishwa kuwania uchaguzi wa urais.

Uamuzi huo ulilaaniwa vikali na vyama vya upinzani, ambavyo vilikata rufaa kuupinga.

Macho na masikio sasa yameelekezwa kwa bwana vita huyo wa zamani, ambaye anaishi uhamishoni Brussels, Ubelgiji iwapo ataamua kumuunga mkono mgombea mwingine kutoka kambi ya upinzani.

Mpaka sasa wagombea wote kutoka kambi ya upinzani wanaonekana kutokuwa na sifa ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho na kuufanya uchaguzi huo kujaa maswali mengi kuliko majibu endapo utakuwa huru na wa haki.

Hiyo inatokana na mgombea wa chama tawala Waziri wa mambo ya Ndani Emmanuel Ramazani Shadary kutopata mpinzani wenye nguvu katika uchaguzi huo, ambao umeahirishwa kwa miaka miwili sasa.

Uteuzi wa Shadary, mfuasi mkubwa wa Kabila umefanya wachambuzi wengi wa mambo waseme kuwa rais huyo aliyeingia madarakani mwaka 2001 kufuatia kuuawa kwa baba yake Laurent Kabla anadhamiria kuwa karibu na siasa za taifa ili kumwekea mazingira ya kuwania tena urais mwaka 2023.

Makamu huyo wa rais zamani, aliyekuwa akisumbua kichwa cha Rais Kabila hivi karibuni aliachiwa na ICC katika kesi dhidi ya uhalifu wa kivita baada ya kukaa jela miaka 10. Hata hivyo, bado anakabiliwa na kesi ya kuhonga mashahidi.

Mwezi uliopita alirejea nchini DRC na kufanyiwa mapokezi makubwa kutoka kwa wafuasi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles