23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YAKUBALI VIPIMO MKOJO WA WEMA

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imekubali kupokea ripoti za mkemia zinazothibitisha kwamba sampuli ya mkojo wa Mlimbwende wa Tanzania 2006, Wema Sepetu, imekutwa na chembechembe za bangi na majani yalibainika kuwa dawa za kulevya aina ya bangi.

 

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, alikubali kupokea ripoti hizo mbili na kuzitambua kama kielelezo namba moja cha upande wa mashtaka, baada ya kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala.

 

Hakimu Simba alisema hakuna ulazima wa ripoti ya mkemia kuwasilishwa mahakamani ikiwa imeambatana na fomu ya maombi iliyotoka Polisi, ikielekeza mshtakiwa afanyiwe uchunguzi.

 

“Kazi ya mkemia ni kufuata maelekezo kwa kuchunguza, Jamhuri ndiyo yenye jukumu la kujua ni nani anayestahili kuitoa fomu hiyo mahakamani kama kielelezo, mahakama imepokea ripoti zote mbili kama kielelezo namba moja,” alisema Simba.

 

Agosti mosi mwaka huu, Mkemia Elias Mulima, akiwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai mahakamani kwamba alivyoufanyia uchunguzi mkojo alibaini mshtakiwa huyo anavuta bangi na akataka kutoa kielelezo ambacho kilipingwa na upande wa utetezi.

 

Wakili Peter Kibatala, anayemtetea Wema, alipinga ripoti hiyo isipokelewe kwa sababu haijakidhi kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

 

Kibatala alidai kuwa, kifungu hicho kinaeleza utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kitabibu kwa mshtakiwa ambaye yupo chini ya ulinzi kuwa ni lazima Polisi awasilishe maombi mahakamani.

 

Kibatala aliomba ripoti hiyo ikataliwe kwa sababu hakukuwa na ombi wala amri kutoka mahakamani.

 

Pia alipinga ripoti hiyo kupokelewa kwa sababu haijaambatanishwa na fomu namba DCEA 001 iliyotoka Polisi kwenda kwa mkemia kuomba mteja wake afanyiwe uchunguzi.

 

Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, akijibu hoja hiyo, alidai fomu  yenye namba 001 inatumiwa na  Polisi wanapopeleka sampuli  na fomu namba 009 ni taarifa ya Mkemia na kwamba fomu moja haitegemei nyingine kwa kuwa zinaandaliwa na watu tofauti.

 

Kakula alidai kuwa, sheria haijasema muda wote ni lazima maombi yapelekwe mahakamani amri itoke ndiyo mshtakiwa afanyiwe mchunguzi wa kitabibu, ila pale ambapo mshtakiwa hataki Polisi wanaweza kufanya maombi mahakamani.

 

Katika ushahidi wake, Mulima alidai Februari 8, mwaka huu, alipokea sampuli ya mkojo wa Wema na Februari 6 alipokea majani ambayo aliyafanyia uchunguzi kujua kama yalikuwa dawa za kuleya ama la.

 

“Wema aliletwa ofisini kwa Mkemia na Inspekta Willy na WP Mary, alipofika nilimfanyia usajili na kumpa namba ya maabara 321/2017.

 

“Walimleta kwa sababu walitaka Wema apimwe mkojo na nilimpa kontena maalumu na kumpatia WP Mary ambaye aliongozana naye hadi kwenye vyoo akatoa sampuli ya mkojo.

 

“Baada ya kupatikana mkojo nilipokea sampuli hiyo na kuendelea na uchunguzi ambapo hatua ya kwanza ni kuangalia chembechembe za dawa za kulevya ndani ya mkojo wa Wema na baada ya uchunguzi nilibaini kuna dawa za kulevya aina ya bangi,” alidai.

 

Mulima aliendelea kudai kwamba, kitaalamu bangi inaweza kuonekana kwenye mkojo ndani ya siku 28.

 

Alidai baada ya kuthibitisha kwamba anatumia bangi aliandaa taarifa ya mchunguzi ambayo aliisaini yeye mwenyewe na ikathibitishwa na Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali Februari 8, mwaka huu.

 

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa, Februari 6 mwaka huu, akiwa ofisini kwake, alipokea kielelezo kutoka Jeshi la Polisi Tanzania kupitia kwa D/Koplo Robert, kikitakiwa kufanyiwa mchunguzi kuthibitisha ni dawa ya kulevya aina ya bangi ama la.

 

Alidai alikipokea kwa njia ya fomu DCEA 001, akakisajili na kukipa namba ya maabara 291/2017.

 

Anadai alifungua na kukuta msokoto mmoja na vipisi viwili, ndani yake kuna majani yadhaniwayo kuwa ni bangi.

 

“Niliyapima na kuyakuta yana uzito wa gramu 1.08, nilifanya uchunguzi kwa kutumia kemikali na kubaini ni bangi,” alidai.

 

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Wema, Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas, ambao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

 

Inadaiwa Februari 4, katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio,  washtakiwa walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Kwa upande wa Wema, yeye anadaiwa kuwa Februari Mosi, mwaka huu, katika  eneo lisilojulikana, jijini Dar es Salaam,  alitumia dawa za kulevya aina ya bangi.

 

Hata hivyo, kesi imeahirishwa hadi Agosti 15 na 16, mwaka huu, kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles