23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yakataa kutoa amri Lissu kukamatwa

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kutoa amri ya kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu  kwa kutohudhuria mahakamani.

Badala yake imewaonya wadhamini wake na kuwataka kutimiza majukumu yao.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alikataa maombi hayo jana baada ya Jamhuri kutaka mahakama itoe amri ya kukambwa kwa mwanasheria huyo mkuu wa Chadema.

Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, alidai mshtakiwa anaonekana akizunguka nchi mbalimbali akitoa mihadhara na huko Ubelgiji anakodaiwa yuko hospitali haijaelezwa yuko hospitali gani na anafanya nini.

“Kama itafaa Mahakama iamuru mshtakiwa Lissu akamatwe maana hayupo hospitali kama inavyodaiwa hapa mahakamani,”alidai.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, akijibu alidai hakuna haja ya kufikia hatua hiyo kwa sababu wadhamini wamefika mahakamani na kueleza mshtakiwa yuko wapi.

“Naomba Mahakama ione ni busara kuwakumbusha wadhamini majukumu yao, mshtakiwa akimaliza matibabu atakuja,”alidai Kibatala.

Hakimu Simba alisema shauri lilifunguliwa Juni 14 mwaka 2016 baada ya muda mshtakiwa wa nne (Lissu) akapata matatizo yaliyomfanya ashindwe kufika mahakamani na wadhamini wake wakakaa kimya.

Hakimu aliwaita wadhamini na kuwahoji kwa nini hawafiki mahakamani.

Mdhamini Ibrahimu Mohammed  alisema “naomba Mahakama inisamehe, naahidi nitahudhuria mahakamani kila tarehe, nilishindwa sababu nilikuwa namuuguza mama yangu ambaye mpaka sasa bado anaumwa.

” Mshtakiwa bado anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji na tarehe 20 mwezi huu wa pili alifanyiwa upasuaji wa 23.”

Mdhamini Robert Katula aliomba radhi kwa kutohudhuria mahakamani na kuahidi kuendelea kuhudhuria.

Hakimu Simba baada ya hoja hizo zote, alisema majukumu ya wadhamini ni kutoa taarifa ya mshtakiwa anapokosekana mahakamani.

“Wadhamini wanaonywa, wajue majukumu yao na kuyatekeleza, karibu miezi minane wadhamini hawafiki mahakamani, ombi la kukamatwa mshtakiwa linakataliwa,”alisema Hakimu Simba.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25 kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo   kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Alidai mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

Lissu yupo nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake   Dodoma wakati akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Dodoma kwa ajili ya matibabu na baadaye akapelekwa katika Nairobi,   Kenya ambako alikaa mpaka Januari 6 mwaka 2018 alipohamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambayo anaendelea kuyapata mpaka sasa.

Kwa siku za karibuni, Lissu alifanya ziara  Ujerumani, Uingereza, Marekani  na kurejea Ubelgiji ambako alifanyiwa operesheni ya 23.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles