25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yaamuru mtangazaji wa televisheni apimwe akili

NAIROBI, KENYA

WAKATI ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ikiamuru, Jaque Maribe ashitakiwa kwa mauaji, Mahakama Kuu ya Milimani jijini hapa jana imeagiza mtangazaji huyo wa televisheni afanyiwe uchunguzi wa akili.

Maribe na mchumba wake wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya msichana mfanyabiashara Monica Kimani.

Jaji Jessie Lessiet, anayeshughulikia kesi za uhalifu katika mahakama hiyo, pia amesema Maribe apelekwe katika Gereza la Wanawake la Lang’ata, Nairobi wakati akisubiri uchunguzi wa afya yake ya akili.

Mshukiwa huyu amekuwa rumande, tangu alipokamatwa Septemba 30 na kuzuiliwa katika Kituo cha polisi cha Gigiri.
“Mshukiwa Jacque Maribe azuiliwe katika Gereza la Lang’ata,” alieleza Jaji Lessiet.

Hilo linakuja baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuagiza mapema jana kuwa Maribe ashitakiwe sambamba na mchumba wake, ambaye ni mshukiwa mkuu.

DPP alidokeza kuwa amepokea ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka wawili hao kwa kuhusika kwa njia moja ama nyingine kumuua Monica.

Kwa kawaida, kesi za uhalifu zinazohusu mauaji, mahakama huagiza washukiwa kufanyiwa uchunguzi wa akili ili kuona iwapo wana akili timamu, kabla ya kusomewa mashtaka na kufunguliwa kesi.
Maribe atapelekwa katika Hospitali ya wagonjwa wa akili ya Mathari, Nairobi kwa shughuli hiyo.

Wakili wake Katwa Kigeni alijaribu kuishawishi korti imsomee mashtaka kabla ya kuchunguzwa akili, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba.

Upande wa mashtaka umemwambia Jaji Lessiet kuwa mshukiwa Irungu alishafanyiwa uchunguzi wa akili, na kuonekana kuwa timamu kusomewa mashtaka na kufunguliwa kesi.
Lakini Lessiet ameamuru wawili hao warejeshwe kortini Jumatatu ijayo, ambapo Irungu ataendelea kuzuiliwa katika selo za kituo cha polisi cha Muthaiga, Nairobi.

Irungu anashukiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani (28), alipatikana akiwa ameuawa Septemba 20, 2018 kwenye nyumba yake huko Kilimani mjini hapa.
Marehemu alizikwa nyumbani kwao Gilgil, kaunti ya Nakuru.

Mfanyabiashara huyu alitokea Juba, Sudan Kusini kabla ya kukumbana na mauti aliporejea Kenya akitarajiwa kusafiri Dubai kwa likizo.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari mapema jana, DPP Haji alisema amepitia ushahidi uliopo na kuona unaruhusu wawili hao kufunguliwa mashtaka.
“Kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia kesi na kuwashtaki kwa mauaji, kwa mujibu wa sheria,” alieleza Haji kwenye barua yake.

Akifafanua maelezo ya vipengele 203 na 204 vya katiba vinavyoeleza kuhusu kesi za uhalifu, DPP alisema anayepatikana na kosa la mauaji sheria imeweka wazi anapaswa kutumikia kifungo cha maisha gerezani.

Awali ilikuwa ikielezwa Maribe huenda akashitakiwa kwa shitaka jepesi la kusaidia mauaji, lakini wapelelezi wameona ni vyema kuiachia mahakama iamue.
Hata hivyo, shitaka dogo kama hilo ni uhalifu mkubwa, ambao adhabu yake ni kifungo cha maisha, kwa mujibu wa kifungu 222 vya kanuni ya adhabu.

Hilo linakuja huku rafiki mkubwa wa Irungu ‘Jowie’ na Maribe, Bryan Kassaine akielezwa kuwa anatarajia kutoa ushahidi dhidi ya wapenzi hao.
Wapelelezi na waendesha mashitaka wameona kuwa na shahidi muhimu kama huyo kutawapa imani katika kesi yao hiyo.

Kassaine ni jirani wa Maribe na rafiki wa karibu wa wenzi hao.
Kuna uwezekano Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, George Kinoti atatumia ushahidi wa Kassaine kujaribu kuwahusisha wawili hao na jinai na kile wapelelezi walichoeleza jaribio la kutaka kuficha uhalifu.

Waendesha mashitaka wanatumaini Kassaine ataisaidia mahakama kutambua mtu au watu waliohusika kuchoma moto nguo alizovaa Jowie siku ya mauaji katika harakati za kuficha ushahidi.

Pia wanatarajia kumtumia Kassaine kutoa ushahidi kuhusu silaha yake, Ceska, ambayo ilitumika katika jaribio la Jowie la kutaka kujiua ndani ya makazi ya Maribe Ijumaa Septemba 21
Mtangazaji Maribe alikamatwa Septemba 30 na bado yu kizuizini katika selo za kituo cha polisi cha Gigiri, Nairobi. Irungu, alitiwa mbaroni Septemba 25, na anaendelea kuzuiwa katika selo za kituo cha polisi cha Muthaiga, Nairobi.

Monica alipatikana ameuawa mnamo Septemba 20, 2018 kwenye nyumba yake katika mtaa wa kifahari wa Kilimani, jijini Nairobi.

Marehemu alizikwa nyumbani kwao Gilgil, kaunti ya Nakuru. Familia na wananchi wanataka haki itendeke kufuatia mauaji hayo ya kinyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles