30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Tumeamua

Elizabeth Hombo Na Andrew Msechu

RAIS Dk. John Magufuli, ametaja zaidi ya miradi 20 inayotekelezwa na Serikali, huku akisema licha ya wakati mwingine wahisani kunyima misaada, Serikali imeamua kutekeleza miradi mingi kwa fedha za ndani.

Aliyasema hayo jana Dar es Saalam wakati akizindua jengo la tatu la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lililogharimu Sh bilioni 710.

Rais Magufuli aliwataka Watanzania kujivunia mafanikio hayo na kwamba kufanikiwa mradi huo na mingine ambayo Serikali ya awamu ya tano inaitekeleza, ni kutokana na usimamizi mzuri na nidhamu ya Serikali katika matumizi ya fedha za umma.

“Ndugu zangu Watanzania tunaweza, kinachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya, bila kuamua Watanzania tutaendelea kuwa wategemezi katika miradi ya maendeleo ya taifa letu.

 “Siwezi nikasimama mbele za watu nikasema haya ni kwa sababu yangu, mimi ni dereva tu, lakini pia huwa ninajiuliza ikitokea siku Mungu akanichukua hao watakaokuja watayamaliza kweli.

“Kwa sababu panahitaji moyo, unafanya hivi huku unatukanwa, lakini inabidi ufanye kwa ajili ya Watanzania, inahitaji kujitoa sadaka ya kweli.

“Ninamshukuru Mungu kwa kuendelea kulisimamia taifa hili na ninawashukuru Watanzania wenzangu kwa kuendelea kuniombea na kunipa moyo, nchi yetu sasa imekuwa ya mfano, watu wanatuogopa sasa, wapo wanaouliza mnapata wapi fedha, mimi ninasema zilikuwa kwa mafisadi sasa zinaenda kwa Watanzania.

“Na hili nataka niwaambie kwa dhati bila woga wowote, kwamba tuliomba fedha kwa ajili ya barabara nne kutoka Ubungo kwenda Kibaha kilometa 20, tukawaomba wafadhili, wametuzungusha zaidi ya miaka miwili, sitaki kuwataja, nikasema tutajenga wenyewe njia nane kwa hela yetu, sasa wametushangaa kwamba fedha tunaipata wapi. 

 “Tumeshapata fedha dola zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kujenga uwanja mkubwa sana wa Msalato na tumeshapata fedha zaidi ya Sh bilioni 410 kwa ajili ya kujenga barabara ya kilometa 110 pale Dodoma.

“Tanzania tunaweza; miradi ya maji ningeitaja hapa ni mabilioni ya fedha, kuna miji zaidi ya 27, Dar es Salaam hapa tumeanza kuboresha masuala ya maji, tumebana mianya ya ufisadi,” alisema Rais Magufuli.

MIRADI 

Rais Magufuli pia alitaja miradi mikubwa ambayo Serikali yake inaitekeleza ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), akisema unatumia Sh trilioni 7.5, mradi wa umeme wa Rufiji Sh trilioni 7.5, ujenzi wa barabara ya juu ya Ubungo Sh bilioni 247.

 Miradi mingine ni daraja ya Kigongo- Busisi mkoani Mwanza Sh bilioni 696.2, daraja la Salender Sh bilioni 270, barabara ya njia nane Kimara Sh bilioni 140, barabara nchi nzima zenye Km 2,115 zinazoendelea kujengwa Sh trilioni 5.37.

“Yote haya ni kwa sababu Watanzania tuliamua, viwanja vya ndege 15 kukarabati na kuvijenga Sh trilioni 1.868. Tumeamua kununua na kujenga rada 4 Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro Sh bilioni  67.3, ni uamuzi wetu.

“Meli Ziwa Victoria na Nyasa Sh bilioni 172.3, Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga Sh trilioni 1.2, kununua ndege nane mpya Sh trilioni 1.03 na sasa tumeagiza nyingine tatu maana yake sasa tutakuwa na ndege 11.

“Tumehamia Dodoma ili kusudi Dar es Salaam iwe mji wa biashara. Tumeamua miradi ya barabara hapa Dar es Salaam, kwa mfano kila eneo ambalo mnaona barabara za lami zinajengwa, jumla tunatumia Sh bilioni 660.

“Tumeamua uwezeshaji wa vijana kina mana na walemavu, mpaka leo katika makundi hayo matatu zimeshatolewa Sh bilioni 54, kujenga miundombinu katika majiji, halmashauri, manispaa Sh trilioni 1.35 zinatumika.

“Miundombinu katika afya kuna vituo vya ujenzi 352, zahanati 30, hospitali 67, ukarabati wa hospitali za zamani 21 jumla yote zimetumika Sh bilioni 321.6. Ununuzi wa vifaa vya hospitalini Sh bilioni 64.

“Katika elimu ukarabati wa shule kongwe 62, ujenzi wa madarasa, maabara nyumba za walimu Sh bilioni 308.1 zimetumika, mikopo ya elimu ya juu Sh trilioni 1.62 zimetumika, elimu bure Sh bilioni 945.87, fedha za kununulia dawa, miradi ya maji, umeme, kilimo, mazingira, miradi ya maliasili yote yametumika mabilioni ya hela ambayo yote siwezi kuyataja,” alisema Rais Magufuli.

TERMINAL III 

Akizungumzia kuhusu jengo hilo la tatu la JNIA, alisema ni mali ya Watanzania na litakuwa likitumiwa na abiria wanaokwenda na kutoka nje ya Tanzania.

Alisema kukamilika kwa jengo hilo kutachangia kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.

Vilevile alisema katika majengo mawili yaliyopo hadi sasa, moja lina uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 na la pili milioni 1.5 huku hilo la tatu likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.

“Jengo hili nimeambiwa linaweza kuhudumia abiria 2,800 kwa saa, haya ni maendeleo makubwa sana kwa taifa na limegharimu zaidi ya Sh bilioni 710. Ninamshukuru Jakaya Kikwete (rais mstaafu) kwa kuanzisha mradi huu, mimi nimekuja kukamilisha tu.

 “Watanzania tunaweza kama tutaamua na kuthubutu, tumeamua na tunaendelea kuamua. Ni heshima ya mradi huu uende kwa Watanzania wenyewe na miradi yote inayotekelezwa ni ya Watanzania.

“Nataka kuwaambia kujiita masikini tukutupe, nchi yetu ni tajiri ila tulitaka kuaminishwa na watu waliotaka kujimilikisha. Kila palipo na nia Mungu yupo na ndugu zangu Watanzania Mungu yupo pamoja na sisi.

“Mradi huu ulisimama kwa sababu mkandarasi alikuwa akitudai, nawapongeza Tanroads pamoja na wizara husika, niseme tu kwa uwazi kwamba TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege) walishindwa kusimamia mradi huu na ndiyo maana tukaamua viwanja vya ndege vyote nchini visimamiwe na Tanroads kama ilivyokuwa zamani, kwa hiyo Mfugale (Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini – Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale) na watu wako hongereni sana na wizara pamoja mkandarasi,” alisema.

Alisema jengo hilo limejengwa kwa gharama kubwa, hivyo litunzwe. 

“Jengo hili limejengwa kwa gharama kubwa sana, tulitunze. Mara nyingi tunapopata miradi kinachofuata ni uharibifu, naomba watakaohusika hapa pamoja na Watanzania wote watakaotumia hili jingo tulitunze, tusiliharibu. 

“Ninafahamu patakuwepo na maduka na mabenki na huduma zingine mbalimbali, Wizara ya Uchukuzi  hakikisheni hayo yanapewa kwa wazawa, hatuwezi kujenga jengo kama hili halafu maduka yamilikiwe na watu ambao sio wazawa,” alisema.

MWENDO WA PUSH-UP

Mara baada ya kufika kwenye sherehe hizo za uzinduzi, Rais Magufuli aliungana na waimbaji wa bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) waliokuwa wakiimba kisha kupiga push-up.

Awali, Rais Magufuli alibaki jukwaani, wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wengine waliposhuka na kucheza kisha kuwatunza wanamuziki hao.

Baada ya kurudi jukwaani kwa viongozi hao, Rais Magufuli ambaye alionyesha kufurahishwa na wimbo uliokuwa ukimsifia tangu awali, alionyesha kuvutiwa na hatua ya wacheza shoo wa bendi hiyo kupiga push-up, mtindo aliokuwa akiutumia katika kampeni zake za mwaka 2015.

Rais Magufuli alinyanyuka katika kiti chake akiongozana na Spika wa Bunge, Job Ndugai na kushuka moja kwa moja, akiungana na wacheza shoo hao kisha kupiga push-up 10 mfululizo.

MFUGALE AELEZA SABABU JENGO KUSIMAMA

Awali Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mfugale, alieleza sababu ya ujenzi wa jengo hilo kusimama mwaka.

Mfugale alisema sababu hiyo ni mkandarasi kudai kiasi cha fedha kilichokuwa kimebakia huku akiwa amefanya kazi kwa asilimia 55.

Alisema hadi mwaka 2016, mkandarasi huyo ambaye ni Bam International ya Uholanzi alikuwa amelipwa Sh bilioni 380 na kudai Sh bilioni 29.

Mfugale alisema Februari 8, mwaka juzi baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika jengo hilo, alishangazwa na gharama hiyo na kuagiza kufanyika kwa mapitio ili kuona kama ni halisi.

“Uliagiza (Rais Magufuli) mara moja kuwepo timu ya wataalamu iliyogundua fedha hizo zimelipwa na hata mkandarasi angesimamishwa ingekuwa hasara kwa Serikali na ukaamua kutoa fedha yote ambayo mkandarasi alikuwa anadai ndipo akarudi na leo tuko hapa. 

“Hadi kukamilika kwa jengo hili, mkandarasi amelipwa Sh bilioni 687.4 wakati mshauri mwelekezi akilipwa Sh bilioni 13.1 na ujenzi kwa ujumla ulikadiriwa kugharimu Sh bilioni 705.

“Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 560 zinatokana na mkopo kutoka Hongkong and Shanghai Bank Corporation (HSBC) ya China,” alisema Mfugale.

SPIKA NDUGAI

Akizungumza katika uzinduzi huo, Spika Ndugai alisema wakati uwanja huo wa kisasa ukiwa umeboreshwa, ipo haja ya kuangalia namna ya kuboresha utalii wa pwani ya bahari, kama ambavyo nchi jirani ya Kenya imekuwa ikifanya kuanzia Mombasa, Malindi hadi Lamu.

Alisema nchi hiyo imeimarisha eneo la pwani na kulifanya kuwa na shughuli nyingi zinazowavutia watalii, ikiwa ni pamoja na kuwa na hoteli za kisasa na kujenga klabu maalumu za michezo ya majini, ikiwemo boti maalumu za mwendokasi na michezo ya kuteleza kwenye maji, ambayo watalii wengi huipenda.

Ndugai alisema Tanzania ina hifadhi za mwambao wa pwani kuanzia Pangani hadi Mtwara ambazo ni bora kuliko zozote katika Afrika ambazo bado hazijapangwa vizuri, kwa kuwa ziko chini ya Wizara ya Mifugo.

Alisema fukwe hizo zikipangwa vizuri zitaongeza idadi kubwa zaidi ya watalii, hivyo ni vyema Wizara ya Utalii na Wizara ya Mifugo zikae pamoja na kuangalia nini cha kufanya kuliweka suala hilo vizuri.

 “Lakini pia tukumbuke kuwa uwanja huu ndio lango kuu la nchi yetu, kwa hiyo kila mtu anapita hapa, kwa unziduzi huu sasa tunakuwa na taswira nzuri, hapa ndipo kunakoonyesha Tanzania halisi ya sasa,” alisema.

JAJI MKUU

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alisema ni vyema wananchi wajitahidi kutatua matatizo yao nje ya mfumo wa mahakama pale inapotokea miradi mikubwa ya maendeleo.

Mamlaka ya TAA

Mkurugenzi Mtendaji wa TAA, Julius Ndyamukama, alisema mamlaka hiyo imeshakamilisha mchakato wa kuhama kutoka sehemu ya pili ya uwanja huo na kuhamia rasmi sehemu ya tatu ya uwanja, baada ya kujaribisha na kuhakikisha kuwa mifumo yake yote inafanya kazi vizuri.

Alisema majaribio ya awali ya uwanja huo yalifanyika Julai 17 mwaka huu, siku ambayo ndege ya Shirika la Ndege Tanzania aina ya Boeing 787-3 Dreamliner ilipokuwa ikizindua safari yake ya kwanza kwenda Mumbai nchini India, majaribio ambayo yamefanyika mara tatu.

“Tunapozungumza leo, tayari mashirika ya ndege ya kimataifa yameridhika na ofisi za mashirika 18 ya ndege kati ya mashirika 23 zimeshahamishiwa katika eneo la tatu la uwanja huu na tayari tumeshasaini mikataba na kandarasi 22 kati ya 34 wanaojihusisha na usafi na usimamizi wa usalama na mifumo uwanjani hapa,” alisema.

Alieleza kuwa wanaishukuru Serikali kwa kuwa Idara ya Utumishi wa Umma tayari imeshafanya usaili na imekamilisha ajira za wafanyakazi 130 kati ya 141 waliokuwa wakiwahitaji kwa shughuli mbalimbali uwanjani hapo.

Ndyamukama alisema pia kuwa tayari wameshakamilisha na kupata hati za kiutendaji katika idara zote muhimu kuendesha shughuli za uwanja huo, ikiwamo Osha na Zimamoto.

Alieleza kuwa tayari ndege zote kubwa zenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 18 zineshahamishiwa katika uwanja huo mpya.

Alisema fedha za awali za kugharamia mafunzio na jengo tayari zimeshatolewa na ndizo zilizoanza kutumika katika hatua zote za awali za uendeshaji uwanja huo.

WAZIRI KAMWELWE

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe, alisema terminal zote tatu, yaani sehemu ya kwanza, ya pili na ya tatu zitakuwa na uwezo wa kupitisha abiria milioni nane kwa mwaka na kwa sasa zinapitisha abiria milioni tano.

Alisema ongezeko la abiria liko kati ya asilimia 2.5 hadi 3 kwa mwaka, kwa hiyo wataongezeka kwa kasi sana ndani ya muda mfupi, hivyo zitajaa.

Kamwelwe alisema ni vyema kuangalia namna ya kukarabati Terminal II ambayo sasa ina uwezo wa kubeba abiria milioni moja na nusu hadi milioni tatu ili ipendeze na mwaka huu wa fedha atatafuta mshauri atakayesanifu ili kuona namna ya kupanua kiwanja hicho.

Alisema wamepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kujenga kiwanja cha Msalato, wamemaliza kukarabati njia za ndege Mwanza na mwaka huu wataanza kujenga jengo la abiria Mwanza na Agosti watasaini mkataba wa kukarabati uwanja wa ndege wa Songwe.

HISTORIA YA JENGO

Jengo la Terminal III lilianza kujengwa mwaka 2013 na awali ujenzi ulipangwa kutekelezwa kwa Sh bilioni 705.3, lakini kutokana na kubadilika kwa taratibu za kikodi, mchoro wa mradi, gharama ya mradi huo iliongezeka kwa Sh bilioni 85.3.

Wakati mradi unaanza, ulitarajiwa ungekamilika Desemba mwaka juzi, baadaye ukaongezewa mwaka mmoja hadi Desemba mwaka jana, lakini haukukamilika badala yake umekamilika Mei mwaka huu.

Kampuni iliyotekeleza mradi huo ni BAM International ya Uholanzi ambayo ndiyo iliyofanya kazi za ukandarasi na Arab Consulting Engineers (ACE) ya Misri, ilifanya kazi za ushauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles