24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI, MUSEVENI WAAGIZA MAWAZIRI KUONGEZA BIASHARA

Na MWANDISHI WETU, Uganda

RAIS Dk. John Magufuli na mwenzake Yoweri Museveni wa Uganda wamewaagiza mawaziri wa nchi hizo mbili kuongeza biashara ili kupata manufaa ya uhusiano na ushirikiano uliopo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na marais hao,  baada ya kufanya mazungumzo rasmi na kisha kuzungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ndogo ya Masaka, nchini Uganda, ambako Magufuli ameendelea na ziara yake rasmi ya ya siku tatu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema katika msisitizo wa agizo hilo, Magufuli alisema biashara kati ya Tanzania na Uganda ni takriban Sh bilioni 200 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Tumewaagiza mawaziri na wataalamu wakae na waangalie vikwazo vyote vinavyosababisha tufanye biashara kwa kiasi kidogo, wakishajadili watatuambia tufanye nini, tunataka kuona biashara ya Tanzania na Uganda inakua, hivi sasa Uganda imewekeza Dola za Marekani milioni 47 tu nchini Tanzania na kuzalisha ajira 146,000, kiasi hiki ni kidogo sana, ni lazima tuongeze,” alisema Magufuli.

Kuhusu hatua ambazo nchi imechukua, Magufuli alisema pamoja kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, yenye umbali wa kilomita 726, lakini Serikali imekarabati reli iliyopo.

Alisema hilo lilikwenda sambamba na ukarabati wa kivuko cha mabehewa ya treni cha Umoja katika Ziwa Victoria, ili kuwezesha mizigo ya kutoka Bandari ya Dar es Salaam kufika Kampala kwa gharama nafuu, huku ikiendelea kujenga na kuimarisha barabara za mpakani.

“Napenda pia kukushukuru Rais Museveni kwamba Serikali yako sasa itajenga kipande cha kilomita 11 za reli kutoka Portbell hadi Kampala, na sisi tumeamua kuweka bandari kavu pale Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda wasisumbuke kwenda hadi Dar es Salaam, mizigo yao wataipata Mwanza, hii ni njia ya uhakika na nafuu ya kusafirisha mizigo” alisema Magufuli.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Magufuli alisema Tanzania imejipanga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Uganda kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inakwenda vizuri, ukiwamo kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post –OSBP) na mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Kwa upande wake, Museveni, pamoja na kupongeza juhudi za Magufuli za kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi, pia alimuagiza Waziri wake wa Ujenzi na Uchukuzi, Monica Ntege, kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kipande cha reli cha kilomita 11 kutoka Bandari ya Portbell hadi Kampala, ili usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam uanze.

Museveni alisisitiza kukuzwa kwa biashara katika ya nchi hizo mbili, hasa wakati huu ambao Uganda inahitaji kununua gesi ya Tanzania kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha historia ya kuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa kutoka hapa.

Awali, marais wote wawili walishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji la Uganda (UBC) na makubaliano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles