31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli awatisha wakuu wa mikoa, wilaya

1ABRAHAM GWANDU NA JANETH MUSHI, ARUSHA

RAIS John Magufuli amewaambia wakuu wa mikoa na wilaya wajiandae kuwajibika endapo maeneo wanayoongoza yatakuwa na ukosefu wa chakula na kusababisha wananchi kukumbwa na njaa ilhali maeneo mengi ya nchi yamepata mvua za kutosha.

Pia alisisitiza ahadi yake kuwa ataendelea kutumbua majipu yanayonuka, yasiyoiva na vipele vinavyoota hata kama yatakuwamo ndani ya vyama mbalimbali vya siasa ikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana akiwa katika mavazi ya kijeshi maarufu kwa jina la kombati, wakati akiwa njiani kuelekea katika shughuli ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyofanyika wilayani Monduli na kila alipopita katika maeneo mbalimbali wananchi walifunga barabara na kutaka awasalimie.

Shughuli hiyo ni hitimisho la Shughuli ya Onyesha Uwezo wa Medani, Brigedia 303 inayotangulia shughuli ya leo ya kutoa nishani kwa maofisa wa JWTZ.

“Niombeeni, nina kazi ya kutumbua majipu makubwa yanayonuka yale madogo na vipele hata katika vyama vya siasa ikiwemo CCM,” alisema Magufuli huku akishangiliwa na wananchi waliozuia njia eneo la Kona ya Chuo cha ufundi Arusha.

Alisema hawezi kukubali kuona wananchi wanakufa kwa njaa na wakifa atakayewajibika ni mkuu wa mkoa husika.

Pia aliwaambia wananchi wamwamini kuwa yeye ni rais asiyebagua wananchi wala itikadi za vyama ndiyo maana anawaomba ushirikiano na wazidi kumuombea ili aendelee kupasua majipu.

Pia baada ya kuanza safari yake katika eneo la Mount Meru, Magufuli, alilazimika kusimama mara kwa mara katika maeneo hayo, Tenki la Maji, Mianzini na Tekniko na aliwasisitiza wananchi kuendelea kumwombea ili aweze kuleta maendeleo.

Alipofika eneo la Ngarenaro kutokana na wingi wa watu alisimama na kusikiliza kero za wananchi na miongoni mwa kero hizo ni manyanyaso wanayopewa wananchi katika Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso ikiwemo na kesi za mirathi katika mahakama mbalimbali kuchukua muda mrefu pia wananchi wanadaiwa rushwa katika Hospitali ya Mount Meru.

“Tuna kilio, rais tunaomba utusaidie mahakama ya mwanzo rushwa imekithiri, pia kesi za mirathi zinachukua muda lakini pia rushwa katika Hospitali ya Mount Meru tunaomba baba utusaidie,” alisema mmoja kati ya wananchi waliosimama barabarani ambaye hakutaja jina lake.

Pia eneo la Kona ya Nairobi alisimama na kusoma mabango yaliyokuwa yakimtuhumu Diwani wa Kata ya Ungalimited kwa kuendekeza siasa za vyama huku mengine yakieleza kero za ushuru na tozo mbalimbali katika masoko ya Jiji la Arusha.

Baada ya Magufuli kusoma mabango hayo na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo aliyokuwa akipita, alisema kero hizo anaziwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, aliyekuwa pamoja naye katika msafara wake.

“Leo nipo vizuri kikombati na hizi kero mlizozisema kwa sababu bado nipo hapa mkoani Arusha nitakaa na Ntibenda ili kuhakikisha zinatatuliwa na nitazikabidhi kwake lakini nawaomba mzidi kuniombea ili niweze kuwatumikia katika kipindi hiki ninachoongoza.

“Nawashukuru wananchi wa Arusha kwa  kujitokeza kwa wingi barabarani na kunipokea na leo nawasalimia tu na nitapanga siku ya kuja kuongea na nyinyi hapa Arusha,” alisema Magufuli.

Pia alisimama Kona ya Mbauda, Majengo na Kisongo na baadhi ya wananchi katika maeneo hayo walisema walijitokeza njiani kumpongeza kwa sababu ameonyesha kwa moyo wa kipekee jinsi anavyoweza kufanya kazi ikiwemo kukusanya mapato ya Serikali yaliyokuwa yakiibwa na watu wachache.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles