25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI ANAJINASISHA KWENYE MTEGO ALIOUKWEPA MWANZONI?

ALIPOUNDA baraza la mawaziri la kwanza na kuwataja mawaziri 19, Rais John Magufuli alisema ameamua kuunda baraza dogo ili kubana matumizi ya Serikali. Alisema kuwa anataka Serikali yake ioneshe kubana matumizi kwa vitendo. Kama ilivyo kawaida,maoni yakatolewa mengi.

Kabla ya uteuzi huo, wapo ambao walishauri kuhusu ukubwa wa baraza la mawaziri wakisema gharama za uendeshaji wa Serikali zisitumike kama kigezo kikubwa cha ukubwa wa baraza. Walisema ukubwa wa baraza unapaswa kutokana na ajenda ambazo Serikali imepanga kuzitekeleza. Walisema hata kama baraza likiwa kubwa, kama litakuwa na ufanisi, gharama zake zitamezwa na uzalishaji.

Baada ya uteuzi wa kwanza wa Rais Magufuli, waliibuka watu waliosema kuwa baraza hilo bado ni kubwa. Wakasema angeweza kuteua mawaziri 15 tu na wakafanya kazi nzuri sana.

Lakini wapo ambao waliona kuwa baraza hilo ni dogo mno kulinganisha na ajenda ambayo Serikali ilikuwa inataka kuitekeleza. Wakashauri kugawanywa kwa baadhi ya wizara ili kuhakikisha kazi katika sekta husika zinafanyika kazi kwa ufanisi. Kama kawaida, Rais Magufuli akaendelea na kazi yake ikiaminika kuwa ameamua kutotilia maanani ushauri huo.

Takribani miaka miwili baada ya kuendesha Serikali, juzi Rais Magufuli alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri, akizigawa wizara mbili na hivyo kuwa na jumla ya wizara 21 na pia akiteua manaibu mawaziri wengi.

Kinachojionesha hapa ni kuwa baada ya kuona uzito wa ajenda ambayo Serikali inapaswa kuitekeleza, Rais Magufuli amebaini kuwa ukubwa wa Baraza, hasa kwa maana ya kupunguza gharama, si kigezo kizuri sana. Amebaini kuwa kuna mambo ambayo hayaendi kwa jinsi ambavyo angependa yaende na hilo linatokana na kukosekana kwa watu wa kutosha wa kutekeleza ajenda hiyo.

Inavyoonekana Rais Magufuli amebaini kuwa wale wachache waliopo wana majukumu mengi sana kiasi kuwa inakuwa vigumu kwao kuwa na tija kubwa.

Katika mazingira kama hayo, Rais Magufuli atakuwa amefanya vyema sana kuamua kutekeleza ushauri aliopewa na baadhi ya watu kuhusiana na muundo wa Serikali yake, ingawa ametekeleza baada ya yeye mwenyewe kujionea jinsi ilivyo vigumu kutekeleza ajenda zake kulingana na maono yake ya awali.

Lakini uamuzi wa kubadili muundo wa Serikali kwa kuongeza wizara mbili ni jambo moja. Kuhakikisha kuwa wizara hizo mpya zinafanya kile ambacho Rais Magufuli amekusudia zifanye ni jambo jingine. Tuangalie mfano wa wizara ya kilimo.

Naamini lengo kubwa ni kuhakikisha kilimo kinakua. Lakini kama tukidhani kuwa kugawanywa tu kwa wizara kutatufikisha pale tunapotaka, tutakuwa tunajidanganya. Ili kuinua kilimo tunalazimika kwanza kuanza na kubadili mawazo yetu kuhusu kilimo – kutoka kukiona kilimo kama shughuli iliyodharaulika na dhalili mpaka kukiona kilimo kuwa shughuli muhimu katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Mkazo unaowekwa kwenye sekta nyingine kama vile ujenzi wa viwanda na madini unapaswa pia kuwekwa kwenye kilimo. Kuwe na juhudi za makusudi za kivitendo zitakazowawezesha watu kuona kuwa kweli kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

Na ili kulifanya hilo, Serikali isione aibu kuwekeza kwenye kilimo. Ili kufanikisha hilo Serikali isione aibu wala woga kutoa vishawishi kwa watu, taasisi au kampuni zilizo tayari kuwekeza katika sekta ya kilimo. Kilimo hakitakuzwa kwa maneno maneno tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles