MAGUFULI AMKAANGA MAKONDA SAKATA LA MAKONTENA, AMTAKA KUYALIPIA KODI

0
757

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais John Magufuli amepigilia msumari sakata la makontena ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kumtaka kuyalipia kodi.

Aidha, amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamisi Agosti 30, wilayani Chato mkoani Geita, wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo.

“Viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi, kwa mfano mgogoro wa makontena yanayodaiwa kuwa na fenicha za shule yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Bandari ya Dar es Salaam, nasema makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria.

“Eti Mkuu wa Mkoa ameleta makontena anaambiwa alipe kodi hataki, kwa nini asilipe kodi, kwa sababu ni mtu mmoja tu  katika nchi hii kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6,13 na 15 Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali hakuna mtu mwingine, hayupo.

“Kwa msingi huo, hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo.

“Labda umezungumza na watu wengine na wafanyabiashara unasema una makontena yako halafu ukasema ni ya walimu halafu hata shule hazitajwi maana yake nini, maana yake si unataka utumie walimu upelek kwenye shule tatu mengine upelek kwenye shopping mall, kwa hiyo wafanyakazi waitumike kwa maslahi fulani,” amesema Rais Magufuli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here