26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli aliweka tayari jeshi sakata la korosho

Na MWANDISHI WETU -Dar es Salaam


RAIS Dk. John Magufuli amekagua magari ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yaliyoandaliwa kubeba korosho endapo wanunuzi hawatotii agizo la kuzinunua ifikapo kesho saa 10 alasiri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli alifanya ukaguzi huo katika Kambi ya Jeshi ya Twalipo, Kikosi cha Usafirishaji cha 95KJ Mgulani, Dar es Salaam jana na magari 75 yenye uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,500 kwa wakati mmoja yameandaliwa kubeba korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga.

Akizungumza na maofisa na askari wa JWTZ waliokuwapo wakati wa ukaguzi huo, Rais Magufuli alisema endapo wanunuzi binafsi hawatotii maagizo ya Serikali ya kununua korosho za wakulima kwa bei isiyopungua Sh 3,000 kwa kilo moja na agizo lililotolewa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hawatoruhusiwa kuzinunua.

Alisema Serikali itachukua hatua ya kulitumia JWTZ na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuzinunua zote kwa bei ya zaidi ya Sh 3,000 kwa kilo moja.

Pia alisema baada ya kuzinunua, Serikali itatafuta soko na nyingine zitabanguliwa kwa soko la ndani na nje ya nchi.

“Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho Serikali ipo na itaendelea kuwapigania, ikifika Jumatatu saa kumi jioni, hawa wanunuzi binafsi hawajajitokeza na kueleza watanunua tani ngapi, tutanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo,” alisema.

Rais Magufuli alisema Serikali inalazimika kuchukua hatua hizo baada ya wanunuzi hao kufanya mgomo wa kuzinunua licha ya kufanya nao mazungumzo na kufikia makubaliano Oktoba 28, mwaka huu.

Alisema katika mazungumzo hayo Serikali iliungana na msimamo wa wakulima wa kukataa bei ya kati ya Sh 1,900 na 2,700 kwa kilo moja na kukubaliana kuwa zitanunuliwa kwa bei isiyopungua Sh 3,000 kwa kilo moja.

Pia alisema pamoja na kufikiwa kwa makubaliano hayo, wanunuzi hao wameendelea kutotii kwa sababu kati ya kampuni 37 zilizoomba kununua korosho, 14 tu ndizo zimejitokeza na ununuzi unafanyika kwa kusuasua.

“Nimefurahi sana kwamba JWTZ lipo tayari kufanya operesheni hii na tunaweza kuiita Operesheni Korosho, nimeambiwa kuwa kuna takribani tani 210,000 za korosho, kule Lindi na Mtwara kuna maghala yanayoweza kuhifadhi tani 77,000 na hapa Dar es Salaam kuna maghala yanayoweza kuhifadhi zaidi ya tani 90,000 pamoja na maghala mengine, natarajia kuona zoezi hili linakamilika haraka.

“Na kutokana na jambo hili, sasa JWTZ kupitia JKT ianze kufikiria kuanzisha kiwanda kikubwa cha kubangua korosho, hata kama itakuwa ni kwa Serikali kutoa fedha za kujenga kiwanda hicho, tuanze kuachana na uuzaji wa korosho ghafi, huo ni utumwa, tuwe na viwanda vyetu na vijana wetu wapate ajira,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema yeye ni askari aliyeiva hivyo hatikisiki hata kwa aina yoyote ya upepo na mara nyingi waliojaribu kumtikisa walitikisika wenyewe.

Alisema yeye kama Amiri Jeshi Mkuu anajisikia raha na mwenye furaha kubwa anapokuwa na wanajeshi.

“Mimi ni askari niliyeiva, sitikisiki hata kwa upepo wa aina gani. Mara nyingi waliojaribu kunitikisa walitikisika wenyewe, lakini nafahamu kuna JWTZ ambalo katika historia yake tangu lilipoanza halitikisiki na wala halitegemei kutikisika na kamwe halitatikisika katika maisha yote,” alisema.

Awali akitoa taarifa ya maandalizi ya kutekeleza jukumu hilo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alisema JWTZ imetayarisha magari 75 ya uwezo tofauti yenye uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,500 kwa wakati mmoja na tani nyingine 500 zitabebwa na meli ya kijeshi (landing craft) inayoweza kutia nanga mahali popote katika ufukwe wa bahari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles