27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Magonjwa manne hatari nchi zenye kipato cha kati

moyo ugonjwa

Na Veronica Romwald – Dar es Salaam

WATAALAMU wa afya duniani wanaonya kuwa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza (NCD’s) yanazidi kuwa tishio ikilinganishwa na yale ya kuambukiza.

Wanasema iwapo hatua hazitachukuliwa basi idadi ya watu wanaougua magonjwa hayo itazidi kuongezeka.

Kulingana na andiko lililopo katika mtandao wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza husababisha vifo vya takribani watu milioni 38 kila mwaka.

Kwa mujibu wa mtandao huo karibu robo tatu ya vifo hivyo sawa na milioni 28 hutokea katika nchi zenye kipato cha kati na chini, Tanzania ikiwamo.

Unafafanua kuwa vifo milioni 16 sawa na asilimia 82 hutokea mapema kabla ya umri wa miaka 70 katika nchi hizo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anakiri kwamba kuongezeka kwa idadi ya watu wanaougua magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza nchini ni changamoto.

“Kuna msongamano mkubwa mno hivi sasa katika baadhi ya hospitali zetu, ni jambo ambalo linaloninyima usingizi natafakari jinsi ya kukabili hali hiyo.

“Lakini kati ya wagonjwa hao tumebaini wengi wao ni wale wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza,” anasema.

Anasema serikali imekuwa ikitumia kati ya Sh bilioni 20 hadi 25 kila mwaka kugharimia matibabu ya watu wanaosumbuliwa na maradhi hayo nje ya nchi.

“Hizi ni fedha nyingi mno, ndio maana serikali inataka kuboresha hospitali zake kuwezesha huduma za kibingwa kama ile Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), zipatikane nchini kwa kiwango kinachofaa ili ipunguze idadi ya wanaopelekwa kutibiwa nje ya nchi.

“Sasa imekusudia kuanzisha ya upandikizaji figo kwa wale ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi na ile ya upandikizaji wa sikio (cochlea) kwa wasiokuwa na uwezo wa kusikia,” anasema.

Magonjwa hatari

Kwa mujibu wa WHO, magonjwa ya moyo, saratani, kupumua na kisukari yanatajwa kuwa ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo vyote vinavyotokana na magonjwa hayo.

Inaelezwa kuwa magonjwa hayo huchangia kwa kiwango cha asilimia 82 kwa vifo vyote vinavyotokana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

Magonjwa ya moyo huua takribani watu milioni 17.5 kila mwaka ikifuatiwa na yale ya saratani ambayo husababisha vifo milioni 8.2.

Mengine ni magonjwa ya kupumua ambayo huua watu milioni nne kila mwaka pamoja na kisukari ambayo huua watu milioni 1.5.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles