26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAGHEMBE: KALAMU ZA WAANDISHI ZIMEBEBA DHAMANA YA UTALII

*Asema bila wao mambo yangekuwa magumu, awapongeza

*Uingizaji wa mifugo hifadhini bado tatizo kubwa, elimu yahitajika

Na Kulwa Karedia

HIVI karibuni Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), iliandaa mkutano wake wa kila mwaka wa kukutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, waandishi waandamizi na wamiliki wa mitandao ya kijamii mkoani Tanga.

Lengo kubwa la kukutana kila mwaka kati ya wahariri na mamlaka hiyo, ni kuelezea changamoto zilizopo na namna ya kuzishughulikia ili sekta ya utalii izidi kujitangaza kitaifa na kimataifa.

Katika mkutano huo, kila upande hutoa mada na michango mbalimbali ili kuona ni wapi panahitaji kufanyiwa kazi zaidi katika sehemu mbalimbali.

PROFESA MAGHEMBE

Akifungua mkutano huo ambao ni  wa sita tangu Tanapa ianzishe ushirikiano wake na vyombo vya habari, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, anasema vyombo vya habari vimefanya kazi kubwa mno hasa wakati wa kupambana na janga la ujangili ambao kwa namna moja au nyingine lilitishia uhai wa hifadhi za Taifa.

“Navipongeza mno vyombo vya habari kwa kazi kubwa ambayo mnaifanyia kazi sekta hii…nakumbuka wakati vita ya kupambana na ujangili ikiwa imeshamiri, mlifanya kila linalowezekana kuwajulisha Watanzania hatua zinazochukuliwa na Serikali.

“Pamoja na pongezi hizi, napenda kutoa rai kwenu kuongeza bidii kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi endelevu wa maliasili za Taifa kwa faida ya jamii iliyopo na vizazi vijavyo,” anasema.

Anasema kuna Watanzania wengi mno hawana utamaduni wa kutembelea hifadhi za Taifa na kuwaachia raia wa kigeni tu, jambo ambalo si sahihi.

“Jitahidini mno kuandika na kutangaza habari hizi ili Watanzania wajenge utamaduni wa kutembelea hifadhi zao…wasiachie wageni tu pamoja  na ukweli kwamba tunawahitaji mno,” anasema Profesa Maghembe.

Kuhusu ujangili, Profesa Maghembe alisema pamoja na kupungua kwa kiwango kikubwa, lakini bado upo na hatua kali zinaendelea kuchukuliwa kila kukicha.

“Ujangili bado upo, majangili tumepambana nao kwelikweli, ninyi wanahabari mmetusaidia katika kuhabarisha jamii juu ya matukio ya kukamatwa kwao na hukumu wanazozipata, jambo ambalo limesaidia kujenga woga kwa watu kushiriki katika vitendo hivi…hili ni jambo la kujivunia mno kwa sababu mnathamini rasirimali zenu,” anasema Maghembe.

Anasema pamoja na kuwapo hofu hiyo na jitihada za Serikali za kupambana na ujangili, kwa namna moja au nyingine  imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ujangili  ambayo yalitishia uhai  hasa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ambapo mizoga mingi ya tembo inayotokana na ujangili imepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha ni miaka iliyopita.

Anasema kutokana na hali hiyo, wizara imelazimika kufanya mabadiliko makubwa kwa askari wake katika hifadhi hizo kwa kuwapa mafunzo ya jeshi usu ili waweze kukabiliana na majangili.

“Tumefanya mapinduzi makubwa ya kuwapa mafunzo askari wetu kutoka uraia hadi jeshi usu ili kukabiliana na mbinu za majangili hawa…tunaamini hatua hii itasaidia mno.

“Pamoja na hatua hii, pia tumelazimika kuwa na ndege ambazo hazina rubani (drones), zinasaidia kuzunguka huku na huku, tembo wapo waliofungiwa alama maalumu ambazo hata wakivuka eneo fulani inakuwa rahisi kuwafuatilia,”anasema Profesa Maghembe.

CHANGAMOTO

Kuhusu changamoto zinazozikabili hifadhi zote, Profesa Maghembe anasema tatizo la uingiaji wa mifugo mingi kwenye hifadhi limekuwa kubwa, licha ya hatua kadhaa zinazochukuliwa.

“Pamoja na kuwa na sheria kali za uhifadhi zinazokataza wananchi kuingiza mifugo hifadhini, hali bado si nzuri…tumekamata mifugo mingi katika hifadhi mbalimbali.

“Mifugo bado inaingizwa mno hifadhini, sheria za uhifadhi zinakataza watu kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria, ni wajibu kwa wanahabari kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutii sheria hizo.

“Ni vema wanahabari mkatumia kalamu zenu vizuri kuelimisha jamii juu ya athari za mwingiliano wa binadamu, mifugo na wanyamapori,” anasema Profesa Maghembe.

Akisisitiza umuhimu wa wananchi kutii sheria, Profesa Maghembe anasema wanyamapori wanabeba virusi vya magonjwa mbalimbali, ikiwemo homa ya Bonde la Ufa, ndigana, kifua kikuu, homa za vipindi (brucolosis) na kimeta.

“Kwa kweli magonjwa haya  yanaweza pia kuambukiza mifugo na binadamu wanaoishi karibu na hifadhi za wanyamapori…kama nilivyosema kalamu zenu zikitumika vizuri ni wazi wananchi watatambua umuhimu wa kutii sheria hizi na kutopeleka mifugo tena,” anasema.

Anasema  kama  mwingiliano huo utaendelea kuwapo muda mrefu, unaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa magonjwa kwa binaadamu na mifugo, kitendo ambacho kinaweza kusababisha vifo vingi kwa wakati mmoja na kuigharimu Serikali.

Kuhusu kumega maeneo ya hifadhi  kwa ajili ya kuwagawia wananchi, Profesa Maghembe anasema jambo hilo halina ukweli wowote.

“Si kweli kumega eneo la hifadhi fulani na kuwapa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo itasaidia kupunguza tatizo hili…nasisitiza hakuna mpango wa aina hiyo hata kidogo…Nasema tena na tena kuwa njia pekee na salama ni kubadili mfumo wa matumizi ya rasilimali zilizopo, ikiwapo ya ardhi kwa kutumia sayansi na teknolojia na kuweka matumizi bora ya ardhi kwa kulenga matokeo chanya.

UTALII

Kuhusu utalii, Profesa Maghembe anasema waandishi wa habari wanapaswa kuwa sehemu ya kukuza uchumi wa nchi kwa kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa taarifa sahihi kwa Watanzania na wageni kuhusu sekta hiyo, bila ubaguzi wa aina yoyote.

“Kila mmoja wenu, aipende nchi yetu, tuitangaze na kuilinda katika habari hizi za uchumi, tuweke itikadi zetu pembeni tuandike habari za kujenga nchi yetu kwa sababu pato la sekta ya utalii ni kubwa katika bajeti ya Serikali kila mwaka”, anasema Profesa Maghembe.

KIJAZI

Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Alan Kijazi, anasema sekta  hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa Taifa kwa kuchangia asilimia 17.2 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.

“Sekta ya utalii imekuwa na mchango mkubwa mno kwa Taifa, utaona asilimia 17.2 si jambo dogo, tungependa kuona tunapita hapo kama ninyi waandishi mtatangaza utalii kwa nguvu zote na sisi upande wetu tunaboresha kila kinachohitajika,” anasema.

Anasema  asilimia 80 ya wageni wanatembelea hifadhi za Taifa, hasa kanda wa kaskazini, jambo ambalo linaweka msukumo wa kuendeleza na kutangaza hifadhi za nyanda nyingine ili kuongeza idadi ya watalii na pato la Taifa.

Kuhusu mchango wa Tanapa katika uchumi wa Taifa, Kijazi anasema umeongezeka ambapo  mwaka 2015/16, ilichangia Sh bilioni 27 katika mfuko mkuu wa Serikali na mwaka 2016/1,7 ilichangia  Sh bilioni 34 sawa na ongezeko la bilioni saba.

“Haya ni mafanikio makubwa ambayo yanaonyesha wazi sekta hii ina mchango mkubwa kwa Taifa…naamini kadiri siku zinavyokwenda nasi tunakimbiza kukamilisha au kukidhi vigezo vinavyotakiwa iwe kwenye hoteli na maeneo mengine ili watalii wasipate shida,” anasema Kijazi.

Anasema pamoja na mafanikio hayo makubwa, jukumu la kuendeleza uhifadhi  haliwezi kufanikiwa kwa jitihada za Serikali pekee bila kushirikisha wananchi kupitia vyombo vya habari.

“Hatuwezi hata kidogo kufanikiwa katika hili bila kushirikisha wananchi kupitia kalamu zenu…natoa rai kwa waandishi wa habari kuiunga mkono Serikali kunadi sera za uhifadhi endelevu kwa masilahi ya Taifa.

“Tanzania ina vivutio vingi vya kipekee ukilinganisha na nchi nyingine duniani, mamlaka kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii na ofisi za balozi zetu nchi mbalimbali, inajitangaza ndani na nje ya nchi ili kuongeza idadi ya watalii,” anasema Kijazi.

Akielezea uvumi kuwa Mlima Kilimanjaro haupo Tanzania, Kijazi anasema hii ni propaganda za ushindani wa kibiashara, lakini matumizi ya teknolojia yamesaidia kutoa elimu na kwamba idadi kubwa ya watalii kutoka nje ya nchi wanaelewa  mlima huo upo Tanzania.

KIBANDA

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wahariri wenzake, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, anasema shirika hilo limepiga hatua kubwa ya kuutangaza utalii, lakini kuna mambo madogo madogo ambayo yanapaswa kurekebishwa.

“Waziri na washiriki nawahakikishia vyombo vya habari vimefanya kazi kubwa mno si kutangaza utalii tu, bali hata wakati wa wimbi la ujangili, tumejitoa na kuandika habari nyingi zikiwamo makala za kuelezea athari za tatizo hili,” anasema Kibanda.

SAADANI

Naye Mkuu Mhifadhi wa Hifadhi Taifa ya Saadani, Dk.James Wakibara, anasema moja ya changamoto kubwa iliyopo ni Watanzania kuwa na mwamko mdogo wa kutembelea hifadhi zao.

“Ukiacha mwamko mdogo wa Watanzania, tuna tatizo jingine la wafugaji wengi kuja na makundi makubwa ya mifugo na kuiingiza katika hifadhi bila kuheshimu sheria zilizopo…tunaamini kupitia mkutano huu mnaweza kutusaidia,” anasema Dk. Wakibara.

RC SHIGELA

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella, anasema mkutano huo ni muhimu kwake kwa sababu umefanyika ndani ya mkoa ambao una vivutio vingi vya utalii.

“Nawaambia hii ni bahati kubwa mkutano huu kufanyika ndani ya mkoa wangu…Tanga hapa tuna vivutio vingi mno ambavyo kwa kweli mkitumia kalamu zenu tutanufaika kama mkoa na Taifa kwa ujumla,” anasema.

Anasema moja ya kivutio kikubwa kilichopo mkoani hapo, ni misitu ya asili ya Amani ambayo iko wilayani Muheza, mapango ya Amboni, Hifadhi ya Taifa ya Saadani na mapango ya Tongoni.

MAAZIMIO

Baada ya mkutano huo, wahariri na waandishi waandamizi  waliazimia maazimio ambayo watayafanyia kazi.

Mosi kuunga mkono juhudi za shirika kutunza hifadhi, misitu na uoto wa asili kwa ajili ya kizazi cha sasa na vile vijavyo, kuendelea kutumia kalamu zao kuelemisha Taifa juu ya umuhimu wa kufanya uhifadhi endelevu wa misitu, wanyama pori na vyanzo vya maji, kupiga vita ujangili na hasa ule wa tembo na faru, kwani unaendelea kumaliza wanyama hao ambao ni adimu na muhimu kwa uchumi wa Taifa, kuendelea kuandika zaidi habari za utalii na hasa vyanzo vya mapato ya utalii ambavyo bado havijulikani kwa umma wa Watanzania ili kuinua mapato ya utalii kitaifa.

Mengine ni shirika kuahidi kuendelea kutoa zawadi kwa waandishi wa habari wanaoandika kwa weledi mkubwa habari zinazohusu uhifadhi, uoto wa asili na utalii na hasa utalii wa ndani, ikiwezekana waandishi wapewe mafunzo zaidi kuhusu elimu ya uhifadhi na utalii ili wafanye kazi zao kwa weledi zaidi, waandishi waandike habari chanya zinazoweza kukuza biashara ya utalii nchini na kuepuka kuandika habari ambazo zinaweza kuathiri biashara hiyo kwa kupunguza idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu, waandishi waandike na kutangaza habari ambazo zitajenga uhusiano mwema kati ya hifadhi za Taifa na wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

Maazimio mengine ni waandishi wa habari kujifunza sheria mbalimbali za misitu, wanyama pori na utalii ili kuwaelimisha wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wa vyombo mbalimbali vya habari, waandishi kujitahidi kuandika habari zitakazopunguza mikwaruzo kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi za misitu na wanyama pori, wataalamu waliowasilisha mada katika warsha hii waendelee kuwasiliana na waandishi waliohudhuria mkutano huo ili habari wanazoziandika ziwe za uhakika zaidi kwa msaada wa kitaaluma kutoka kwao, wahariri kufanya kazi zao kwa weledi na kujiepusha na rushwa inayodhalilisha jamii yetu.

Wasioweza kufanya kazi kwa kufuata maadili waache kazi na kufanya shughuli nyingine, kwa elimu waliyopata kwenye warsha hiyo, mwakani wakati wa kikao kama hicho, kila mshiriki aeleze jinsi alivyoshiriki shughuli za uhifadhi na changamoto alizokutana nazo na shirika hilo lijaribu kuajiri maofisa habari katika hifadhi zote 16 ili kuharakisha mawasiliano na wahariri na waandishi waandamizi.

Akifunga warsha hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, alisema ushirikiano wa wahariri na shirika hilo ni muhimu mno ukaendelea kudumu kwa sababu kila upande wanategemeana.

“Siwezi kuzungumza mengi, nimepitia maazimio mliyokubaliana, napata amani kweli maana nikiongea zaidi nitaharibu mambo mazuri haya,” anasema Waziri Makani.

Katika warsha hiyo, washiriki wote walikabidhiwa vyeti kwa kutambua mchango wao katika sekta ya utalii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles