28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAFURIKO YAUA MAHARUSI WAKITOKA KUFUNGA NDOA

Na JANETH MUSHI-
-ARUSHA

WATU saba wamefariki dunia katika matukio tofauti, kati yao kukiwa na maharusi waliosombwa na mafuriko walipokuwa wakitoka kufunga ndoa ya kimila wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.

Mafuriko hayo yalitokana na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha katika eneo hilo, ambapo maharusi hao wakiwa kwenye gari dogo aina ya Toyota Premio, walisombwa na mafuriko baada ya dereva kushuka ili akapime kina cha maji ili kuona kama angeweza kupita.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea Februari 23 saa 4 usiku katika Kijiji cha Timbolo Kata ya Sambasha wilayani humo ambapo walikuwa wakielekea Kijiji cha Kyoga.

Katika gari hilo, mbali na maharusi hao kulikuwa na ndugu zao wengine watatu ambao pia walipoteza maisha.

Kamanda Mkumbo aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Munisi Loyi (25) aliyekuwa bwana harusi na bibi harusi Nembris Mungaya (20), Inoti George (40), mama mlezi wa bwana harusi, Shengai Saiguran (30) dada wa bwana harusi pamoja na Ngaisi Munuo (11).

Alisema siku ya tukio marehemu hao walikuwa kwenye gari aina ya Toyota Premio lenye namba za usajili T 579 BSG, lililokuwa likiendeshwa na Yusuph Jacobo (35).

Alisema wakati watu hao wakitokea kwenye harusi hiyo, mvua kubwa ilianza kunyesha wakati wakiwa njiani hali iliyosababisha mafuriko hivyo wakalazimika kusimama na ndipo gari liliposombwa na maji.

DEREVA

Akizungumza na waandishi wa habari  nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo, Jacobo, alisema wakiwa njiani kurudi Kyoga, alikuwa akiendesha gari taratibu kwa sababu barabara hiyo ya Timbolo kuelekea Kyoga ilikuwa imechimbwa na greda kwa ajili ya matengenezo.

Alisema kutokana na mvua iliyokuwa imenyesha na maji kutoka mlimani kuwa mengi, walilazimika kusogeza gari pembeni ili kusubiri maji yapungue kwani barabara ilikuwa haina matoleo ya maji wala mitaro hivyo maji yalikuwa ni mengi.

“Tulipofika kwenye kilima maeneo ya kwa Diwani Sabaya, gari ikaanza kuteleza mara ikagonga mti tukatulia pale, mvua ikazidi kunyesha tukaona maji yanayoshuka kutoka juu yatatukuta kwa hiyo tukaamua kusogeza gari upande wa chini kutoka kule juu ili maji yakija yapite pembeni,” alisema Jacobo.

Alisema walivyoegesha gari pembeni, maji yaliendelea kuongezeka na mengine yaliyokuwa yanatoka kwenye kalavati yakaendelea kujaa barabarani hali iliyowalazimu yeye na bwana harusi kushuka kwenye gari ili kurudisha gari nyuma.

“Nilipoona maji ni mengi nikawafungulia milango akina mama nikawaambia washuke ila walipoangalia maji waliogopa, nikaona maji yanazidi nikawasisitiza shukeni shukeni maana nilianza kusikia maji yanatingisha gari ila wakaogopa na nikafungua milango yote ili kuwaokoa ila maji yakazidi yakafunga milango.

“Tukaona maji yanazidi yanataka kuingia ndani ya gari, nikamng’ang’ania kijana wa bodaboda jaketi akanivuta na ghafla  gari likasombwa na maji hadi Mto Selian.

“Wakati huo bwana harusi naye alikuwa nje ya gari ila naye alisombwa na maji wakati gari liliposombwa, inasikitisha sana maana wale ni ndugu zangu,” alisema Jacobo.

Jacobo alisema baada ya wenzake kusombwa na maji, akishirikiana na wenzake wawili waliokuwa kwenye bodaboda, walienda kwa majirani kuomba msaada na kuanza zoezi la kuwatafuta marehemu hao ambao miili yao ilipatikana jana asubuhi kwenye korongo baada ya kuingia kwenye daraja la mto huo.

Mbali na tukio hilo la maharusi, Kamanda Mkumbo aliwataja wengine waliofariki kuwa ni Babu Robikeki (33) aliyesombwa na maji katika Kijiji cha Kerian wakati akiwa anavuka mto.

Alimtaja marehemu mwingine kuwa ni Seuli Meseyeki (37) ambaye ni dereva bodaboda ambaye alisombwa na maji katika eneo la Olorien Ngaramtoni, wakati anavuka mafuriko barabarani.

Wakati huo huo jeshi hilo limeokota pikipiki yenye namba MC 892 ACR aina ya Boxe katika eneo la Kwa Mawala, Kata ya Olasiti, huku dereva wake akiwa hajulikani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles