24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Maduka ya dawa nje ya hospitali kufungwa

mmbandoCHRISTINA GAULUHANGA NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema ipo hatua za mwisho kufunga maduka ya dawa yanayozunguka hospitali zake na vituo vya afya ili kupunguza mgongano wa kimasilahi na wizi wa dawa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Donald Mmbando, alisema tayari wameandaa utaratibu maalumu na shirikishi wa maduka ya dawa ambayo rasimu hiyo ipo hatua za mwisho na atakabidhiwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, atakayeteuliwa kwa ajili ya kuipitisha.

“Baada ya rasimu kukamilika, tutatoa utaratibu ili maduka haya yaondoshwe pembezoni mwa hospitali, na tayari tumeiagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kufungua maduka ndani ya hospitali kadiri wawezavyo, ili wananchi wapate dawa hizo kwa wakati na saa 24 ndani ya siku saba,” alisema Mmbando.

Alisema hali hiyo itasaidia kupunguza wizi wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za Serikali, ikiwa ni pamoja na kuondoa migongano ya kimasilahi.

“Ule wizi wa dawa tunataka ufikie ukomo, ndiyo maana tumeanza utaratibu wa kuweka alama ya TOG katika dawa zetu na tumefanikiwa kwa asilimia 50 hadi sasa, na asilimia iliyobaki tuna imani hadi mwakani itakamilika,” alisema Dk. Mmbando.

Alisema Serikali pia ina mpango wa kutoa bei elekezi ya matibabu katika hospitali za binafsi na za Serikali ili kila mwananchi aweze kumudu gharama hizo.

“Gharama za hospitali zinatofautiana, na hii inachangia wenye kipato cha chini kushindwa kupata matibabu…tumeandaa mwongozo wa malipo wa huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali ambao utasaidia kufahamu viwango elekezi vya gharama hizi,” alisema Dk. Mmbando.

Katika hatua nyingine, Dk. Mmbando amewaagiza wakurugenzi wa hospitali zote za Serikali kuhakikisha wanatenga bajeti kinga ili kumudu gharama za matengenezo pindi vifaa vinapoharibika na kuacha kutegemea Serikali.

“Msisubiri vifaa viharibike, ni vyema wakurugenzi wa hospitali mkawa na mipango ya bajeti kinga ya vifaa vyote katika hospitali zenu ili iwasaidie kukarabati pindi vinapoharibika,” alisema Dk. Mmbando.

Wakati huohuo, Serikali inaendelea na mchakato wa kuagiza vifaa tiba na dawa katika hospitali mbalimbali ili kukidhi upungufu.

Dk. Mmbando alisema kwa upande wa Hospitali ya Saratasi ya Ocean Road, kiasi cha Sh bilioni 4 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambavyo vitatumika katika jengo jipya ambalo linatarajia kukamilika Machi, mwakani.

 

MSD

Dk. Mmbando ameiagiza MSD kuweka dawa za kutosha katika hospitali zote ili kuwaondolea usumbufu wagonjwa wa kwenda kununua nje.

“Naomba iwe mwisho kusikia mgonjwa anaenda kununua dawa nje… eti kisa hospitali hakuna dawa, natamka sitaki kusikia tena, MSD waweke dawa za kutosha na wakurugenzi na kitengo cha manunuzi wahakikishe wanapanga bajeti ili wawe na dawa za ziada.

“Hii ni fursa pekee sasa ya kufahamu bajeti ijayo iongezwe kiasi gani, hasa kwa wagonjwa wa saratani japokuwa na masuala ya kibajeti yanahitaji usimamizi zaidi…jaribu kuvaa viatu vya mgonjwa ambaye anafika hospitali yupo hoi na kuambiwa dawa hakuna…inauma sana,” alisema Dk. Mmbando.

Aliwataka wataalamu wa saratani na wadau wengine kushirikiana kwa pamoja kuendesha kampeni ya tafiti mbalimbali za ugonjwa huo ili kubaini mapema kabla haujafika hatua mbaya ambayo inagharimu mabilioni ya fedha na hata vifo.

“Katika hili naomba ushirikiano hata na watu binafsi …naagiza hili na watakaokiuka maagizo watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema.

 

UNUNUZI WA VIFAA

Dk. Mmbando alisema tayari wamenunua vifaa tiba, ikiwamo mashine za X- Ray nne na Ultra- Sound  zaidi ya 10 ambazo zitagawiwa hospitali mbalimbali.

Alisema hospitali nyingi zinatumia mashine zilizopitwa na wakati, lakini tayari mashine za kisasa zimewasili katika Bandari ya Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles