24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Madudu ya Serikali

mtz1NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

UKAGUZI maalumu uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2014/15 umeibua ufisadi mkubwa katika wizara, idara, wakala za serikali, halmashauri, taasisi na mashirika ya umma.

Katika ukaguzi huo, Wizara ya Ujenzi imegundulika kuwa imefanya malipo hewa ya Sh milioni 951.7 yaliyolipwa kwa
makandarasi kwa kazi ambayo haikufanywa, huku Wizara ya Maliasili ikiwa na malipo hewa ya zaidi ya Sh milioni 156 kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na mgombea urais wa CCM Dk. John Magufuli pia imesababisha hasara ya Sh bilioni 124.8 ambazo ni malimbikizo ya riba iliyozalishwa kutokana na kucheleweshwa malipo ya wakandarasi yenye thamani ya Sh trilioni 5.3.

Katika ukaguzi huo wa PPRA, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ni miongoni
mwa taasisi 17 zilizofanya vibaya katika ununuzi na kuwa na viashiria vya rushwa katika baadhi ya miradi.

Kutokana na ufisadi huo, PPRA imependekeza taasisi zilizohusika na malipo hayo zirejeshe fedha hizo kutoka kwa wazabuni waliolipwa na kuwachukulia hatua za nidhamu watumishi waliohusika na malipo hayo.

Akiwasilisha ripoti ya ukaguzi huo jana, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga, alisema ukaguzi huo ulihusisha taasisi 80 zikijumuisha wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, halmashauri za Serikali za mitaa, taasisi na mashirika ya umma. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mikataba 5,206 yenye thamani ya Sh bilioni 214.6 ilikaguliwa ambako kazi za kandarasi zilikuwa mikataba 345, bidhaa mikataba 1,112, huduma za ushauri wa utaalamu 34, huduma zisizo za ushauri wa utaalamu 1,041, ununuzi yenye thamani ndogo 2,671 pamoja na matumizi ya utaalamu wa ndani mikataba mitatu.

Balozi Lumbanga alisema taasisi 35 zilifanyiwa ukaguzi kupima kama thamani bora ya fedha ilipatikana kwenye miradi 186 yenye thamani ya Sh bilioni 296.

“Ukaguzi huo ulibaini ucheleweshaji mkubwa wa malipo kwa wakandarasi hususan kwenye miradi ya ujenzi wa barabara na miradi ya maji katika Serikali za Mitaa.

Sababu kubwa ni kutokana na ucheleweshaji wa utoaji fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi husika.“Ikumbukwe
kwamba malimbikizo ya riba yataendelea kuongezeka hadi hapo malipo yatakapofanyika.

Unapochelewesha malipo ya wakandarasi halafu yanazaa riba maana yake Taifa linabebeshwa mizigo ambayo
haistahili,” alisema.

“Kati ya miradi 186 iliyokaguliwa, miradi 35 yenye thamani ya Sh bilioni 58.2 ilipata wastani usioridhisha wa chini ya asilimia 50.

“Hii ni ishara kwamba malengo yaliyokusudiwa kwenye miradi hiyo kwa kiasi kikubwa hayatafikiwa na thamani bora ya fedha inaweza isipatikane.

“Miradi 55 yenye thamani ya Sh bilioni 81.26 ilipata wastani wa kuridhisha wa zaidi ya asilimia 75 wakati miradi 96
yenye thamani ya Sh trilion 2.8 ilipata wastani wa kati ya asilimia 50 na 75,” alisema Balozi Lumbanga.

Alizitaja taasisi 17 zilizofanya vibaya na alama zilizopata kwenye mabano kuwa ni NEC (38), TRL (51), Tume ya Ajira
(53), Kituo cha Uwekezaji (51), Shirika la Madini la Taifa-Stamico (56), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (60), Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (56), Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (42), Halmashauri
ya Wilaya ya Karatu (49), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (50) na Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (57).

Nyingine ni Halmashauri za Kigoma (52), Misungwi (55), Iramba (52), Nanyumbu (60), Kyela (60) na Mamlaka
ya Majisafi na Maji taka Lindi (60). “Taasisi hizi zilishakaguliwa miaka iliyopita na kupewa mapendekezo ya namna ya kuboresha ununuzi wao kwa mujibu wa sheria lakini zimeendelea kuyapuuza mapendekezo hayo na kuendelea kufanya vibaya,”alisema.

 

Malipo hewa

Balozi Lumbanga alisema taasisi tisa zilibainika kufanya malipo hewa kwenye miradi yenye thamani ya Sh bilioni 6.4.

“Ukaguzi umebaini malipo ya ziada ya Sh milioni 951.7 yalilipwa kwa wakandarasi kwa kazi hewa, kiasi hiki ni sawa na asilimia 15 ya thamani ya miradi yote ya kazi za ujenzi iliyokaguliwa,” alisema. Mwenyekiti huyo alizitaja taasisi zilizohusika na malipo hewa kwenye mabano kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa – Tanapa (Sh milioni 156.3), TRL (Sh milioni 473.6), Halmashauri ya Kigoma (Sh milioni 11.1), Halmashauri ya Kibondo (Sh milioni 64.9), Halmashauri ya Jiji la Mwanza (Sh milioni 69.6), Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi (Sh milioni 55.6),

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Sh milioni 25.42), Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe (Sh milioni 93.09)
na Halmashauri ya Wilaya ya Kyela (Sh milioni 2.08).

Pia alisema ulifanyika uhakiki wa malipo hewa yaliyobainishwa kwenye ukaguzi wa mwaka 2013/14 na kubaini malipo hewa ya Sh milioni 377. Kuhusu ucheleweshaji wa malipo, alisema mikataba 301 ya Wakala wa Barabara (Tanroads), yenye thamani ya Sh trilioni 5.3 ilicheleweshewa malipo na hivyo kuwa na malimbikizo ya riba ya Sh
bilioni 124.8 hadi kufikia Juni mwaka huu.

 

Rushwa kwenye ununuzi

Kulingana na PPRA, taasisi inapopata asilimia 20 au zaidi katika viashiria vya rushwa ni dalili ya kuwapo vitendo vya rushwa kwenye ununuzi au miradi husika. Kulingana na ripoti hiyo, katika miradi yote
186 iliyokaguliwa, miradi 27 ilibainika kuwa na viashiria vya rushwa kwa zaidi ya asilimia 20 na tayari Taasisi ya Kuzuia ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) imearifiwa ichukue hatua zaidi.

Taasisi tisa zilizobainika kuwa na viashiria vya rushwa ni NEC (asilimia 29), TRL (22), Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (21), Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (22), Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (24), Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (28), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (20), Halmashauri ya Wilaya ya Karatu (31) na Agricultural
Input Trust Fund (28).

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi ni miradi ipi iliyokuwa na viashiria vya rushwa katika NEC, Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk. Laurent Shirima alisema: “Huwezi kutoa taarifa za uchunguzi wowote unaoendelea hadi uwe umekamilika.
“Hatuwezi kutoa taarifa zozote kwa sababu kwa mazingira ya sasa hivi kuna vitu ambavyo huwezi kuvifanya…vinaweza kuwa na madhara au athari kwa jamii”.

 

Hatua zilizochukuliwa

Balozi Lumbanga alisema maofisa masuuli na wakuu wa vitengo wa taasisi 17 zilizofanya vibaya na zilizotekeleza miradi 35 chini ya wastani wa kuridhisha, watawajibika kujieleza mbele ya bodi hiyo kwa nini wasichukuliwe hatua za nidhamu na sheria.

“Mamlaka itachukua hatua ya kuwafungia wakandarasi na wataalamu washauri waliohusika na malipo hewa. Taasisi zote zilizobainika kuwa na viashiria vya rushwa zitawasilishwa Takukuru kwa uchunguzi zaidi.

“Tutapeleka timu ya wataalamu kuhakiki malipo hewa ya wakandarasi kwa kazi ambazo hazikufanywa,” alisema.
Pia alizitaka taasisi 53 zilizopata wastani chini ya asilimia 75 kuwasilisha PPRA mahitaji yao ya mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake.

PPRA pia imezifungia kampuni saba na wakurugenzi wake kushiriki zabuni za umma kutokana na kukiuka mikataba waliyoingia na vitendo vya udanganyifu. Kati ya kampuni hizo, sita zimefungiwa kwa miaka miwili na moja imefungiwa kwa miaka 10 kwa kuwasilisha dhamana za zabuni za kughushi wakati wa michakato ya zabuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles