31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MADUDU MKATABA MLIMANI CITY KUTINGA BUNGENI

NA GABRIEL MUSHI- DAR ES SALAAM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema inaandaa taarifa kamili kuhusu madudu yaliyopo katika mkataba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika mradi wa Mlimani City kisha itaipeleka katika Kamati ya Uongozi ya Bunge kabla haijawahoji wote walioingia mkataba huo.

Hatua hiyo imekuja baada ya wiki iliyopita PAC kubaini kuwa mwekezaji wa Mlimani City alikuja na mtaji wa Dola za Marekani 75 sawa na Sh 150,000 wakati akianza uwekezaji mwaka 2004 na kukiuka taratibu mbalimbali za uwekezaji.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema taarifa hiyo inatarajiwa kujadiliwa na Kamati ya Uongozi ndipo jukumu la kuwahoji waliosaini mikataba hiyo lifuate.

Alisema licha ya viongozi wa UDSM kuhojiwa, pia viongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) waliohusika katika kusaini mkataba huo pia watahojiwa.

“Leo (jana) tunakaa kuandaa taarifa rasmi kuhusu tuliyobaini kwenye mkataba huo, ndipo tuiwasilishe katika Kamati ya Uongozi ambayo sasa itapanga tarehe ya kuwahoji wahusika wa pande zote mbili yaani UDSM na TIC kwa sababu ndio wamehusika kusaini mikataba hii,” alisema Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema).

Mkataba huo wa Mlimani City ulisainiwa mwaka 2004 katika kipindi cha mwisho cha uongozi wa Samuel Sitta, aliyehudumu katika nafasi ya ukurugenzi wa kituo hicho kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2005 na baadaye nafasi yake ikachukuliwa na Emanuel ole Naiko, aliyehudumu kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2011.

Taarifa zinaonyesha walioingia mkataba huo kwa upande wa UDSM ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Mathew Luhanga na aliyekuwa Ofisa Utawala Mkuu wa chuo hicho, Profesa John Mshana.

Waliingia mkataba huo Juni 5, 2004 na wawekezaji (Kampuni ya Mlimani Holdings) ambao ni Gulaam Abdoola na Rizwan Desai.

Kutokana na madudu yaliyogundulika, PAC iliagiza deni analodaiwa mwekezaji huyo lihakikiwe upya na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na lilipwe kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Maagizo hayo yalitolewa na kamati hiyo wiki iliyopita baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ya mradi huo na kueleza kuwa haijaridhishwa na utekelezaji wake tangu mkataba ulipoingiwa mwaka 2004.

Kaboyoka alisema mkataba huo una kasoro kubwa zinazoacha maswali mengi na huenda kuna vitu vimejificha.

MAENEO YENYE UTATA

Kamati ilibaini mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu itakayokuwa na vyumba 100 na bustani ya mimea na wanyama bado haujaanza wakati mkataba unaonyesha inatakiwa ikamilike mwakani.

Alisema awali uongozi wa chuo ulivyoitwa bungeni ulisema mwekezaji amekataa kujenga hoteli hiyo lakini wiki iliyopita walisema hoteli itajengwa.

Eneo jingine lenye utata ni lile la kupunguzwa muda wa mkataba kutoka miaka 50 hadi miaka 35 na kulipwa kwa kodi ya pango kwa ardhi ambayo mwekezaji hataiendeleza.

Kamati ilibaini pia kuna ukiukwaji mkubwa wa malipo ambayo mwekezaji anatakiwa kuilipa UDSM.

Mkataba unaonyesha chuo hicho kinapaswa kipate asilimia 10 ya mapato ya kodi ghafi, lakini mwekezaji hulipa baada ya kutoa gharama za uendeshaji badala ya kuzijumuisha.

Awali Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uwekezaji wa UDSM, Dk. Pancras Bujulu, alisema hadi kufikia Februari, mwaka jana, chuo kinamdai mwekezaji huyo Dola 304,103.46 za Marekani.

Alifafanua kuwa kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka jana, malipo yaliyolipwa na mwekezaji huyo kutokana na pango ni Sh bilioni 16.7 (wastani wa Sh bilioni 1.5 kwa mwaka).

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utawala, Profesa David Mfinanga, alisema tayari wameunda kamati kupitia upya mkataba huo.

MLIMANI HOLDINGS

Taarifa zinaonyesha mwekezaji huyo alitaka kuongezwa jina la UDSM ili mikutano na shughuli za Serikali zifanyike katika kumbi zake lakini chuo kilikataa.

Mwekezaji huyo pia alikataa kupunguza muda wa mkataba kwa kile alichodai kuwa mkopo wa fedha za kuendesha mradi huo umejikita katika kipindi cha mkataba mzima.

Pia walikataa kulipa kodi ya ardhi ambayo haijaendelezwa kwa kigezo kuwa mkataba unawaelekeza kuirejesha kama hawataiendeleza.

Hata hivyo, Meneja Mkuu wa Mlimani City, Pastory Mroso, aliihakikishia kamati hiyo kuwa hadi kufikia mwakani hoteli itakuwa imejengwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles