25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Madudu haya yaliyobainika Hospitali ya Serikali yasiishie hewani

Mwandishi Wetu

Tumeshtushwa na mambo kadhaa aliyoyabaini Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Dk. Faustine Ndugulile katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Dk. Ndugulile ambaye alifanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo alishuhudia yale ambayo yeye mwenyewe ameyaita ni ukiukwaji wa maagizo ya Serikali.

Alikuta kondomu zikiwa zimezagaa na alipomuhoji Mfamasia wa Hospitali hiyo, Elia Kandogo alidai kuwa mipira hiyo ilikuwa imeanikwa kutokana na kuingia maji.

Kiongozi huyo amebaini hayo wakati miezi michache iliyopita mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini iliripotiwa kuwa na uhaba wa bidhaa hiyo.

Lakini pamoja na hayo, kitaalamu kondomu zinatakiwa kuhifadhiwa eneo lisilo na joto kali, vilevile zisiwekwe juani.

Mbali na hilo alikuta dawa zilizokwisha muda wake zikiwa zimehifadhiwa eneo moja na dawa zinazotumika katika stoo ya dawa iliyopo hospitalini hapo. 

Zaidi alibaini hakuna rekodi ya dawa zinazotolewa ambapo alisema kiutaratibu dawa zikitolewa inabidi ziandikwe kwenye kitabu maalumu, lakini katika hospitali hiyo ilionekana dawa zilitolewa bila kuandikwa.

Kutokana na hali hiyo na changamoto nyingine ambazo waziri huyo alizikuta hospitalini hapo aliamuru kuwekwa ndani kwa watumishi wawili, na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Manase Ngogo kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na kushindwa kuwasimamia watumishi wake.

Kilichotushtua sisi ni mambo hayo kukutwa yakifanyika katika hospitali ya Serikali tena chini ya watu wenye ujuzi wao.

Tunajiuliza iwapo wataalamu hao hawajui kwamba kuhifadhi kondomu kwa mtindo huo zinaweza kuwa chanzo cha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini?

Tunajiuliza watalaamu hao hawajui madhara ya dawa zilizokwisha muda wake kiasi cha kuziweka karibu na dawa ambazo matumizi yake hayajaisha, je hawaoni kama katika mazingira hayo wangeweza kuzichanganya na kuzipeleka kwenye matumizi na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa mgonjwa ambaye angepatiwa?

Pamoja na kwamba waziri huyo amekwisha amuru kuwekwa ndani kwa watumishi wawili, na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Manase Ngogo kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na kushindwa kuwasimamia watumishi wake, tuseme wazi kwamba tungekuwa katika nchi inayoheshimu misingi ya afya na sheria jambo hili pengine lingeweza kufika mbali zaidi na pengine leo tungekuwa tunazungumza lugha nyingine.

Kutokana na hayo, sisi tunaona huu ni uzembe wa hali ya juu wa kucheza na afya za Watanzania na haupaswi kuvumiliwa.

Kwa sababu hiyo suala hili lisiishie hewani, ili liwe fundisho kwa wanganga na wauguzi wengine wanaofanya kazi zao kwa mazoea au kutojali na kutozingatia utalaamu.

Tunasema hivyo kwa sababu huenda suala hilo aliloligundua Naibu Waziri katika hospitali ya Rungwe, linafanyika katika maeneo mengine ama kwa mazoea au kwa kutokuwa na watalaamu.

Pamoja na kusisitiza suala hilo lichukuliwe hatua, pia ni vizuri mamlaka husika zikawa zinafuatilia mara kwa mara hospitali, zahanati na vituo  mbalimbali vya afya ili kufahamu changamoto.

Tunaamini hii itasaidia kuzuia tatizo ikiwamo kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza.

Pamoja na hayo, ni vyema mamlaka hizo hizo zikaandaa utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wataalamu wa afya ili kuwakumbusha wajibu wao katika kuzingatia na kutekeleza shughuli za afya kitalaamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles