MADIWANI WENGINE WATANO WAHAMIA CCM

0
317

NA GUSTAPHU HAULE, PWANI              |              


IKIWA ni wiki mbili zimepita tangu gazeti hili kuripoti madiwani 138 wa vyama vya upinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi, idadi hiyo inazidi kuongezeka baada ya wengine watano na wanachama sita akiwamo Ramadhani Lutambi wa Kata ya Mailimoja (Chadema), Kibaha Mjini, kujiuzulu na kujiunga na chama hicho.

Wengine waliohama vyama hivyo ni Rajabu Juma wa Kata ya Mbwawa katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha akitokea Chama cha ACT-Wazalendo, Mharami Mketo (Chadema) wa Kata ya Njopeka Wilaya ya Mkuranga, Seif Rwambo (Chadema) kutokea Mkuranga na Mharami Mkopi (CUF) Kata ya Luaruke, Halmashauri ya Kibiti.

Kadi za madiwani hao zimepokelewa juzi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno, katika ofisi ya chama hicho iliyopo Kibaha Mjini na kuhudhuriwa na wajumbe pamoja na viongozi wa chama hicho ngazi ya kata, wilaya na mkoa.

Akizungumza baada ya kujiuzulu nafasi hiyo, Lutambi, alisema uamuzi alioufanya ni sahihi na hakuna mtu aliyemshawishi isipokuwa amefanya hivyo baada ya kuona Serikali inafanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Nimeamua kujiondoa Chadema na kuvua nafasi zote za uongozi ikiwamo ya udiwani na ile ya ukatibu wa madiwani Mkoa wa Pwani kupitia Chadema na naomba mnipokee kuwa mwanaCCM kuanzia leo (jana),” alisema Lutambi.

Kwa upande wake, Maneno, alisema Serikali imefanya kazi kubwa hasa katika kuwaletea wananchi maendeleo na kudumisha usalama ndiyo maana madiwani na wanachama wengine wa upinzani wanahama vyama vyao.

Aliwataka baadhi ya watu kuacha dhana ya kusema CCM inatoa fedha na kuwanunua madiwani hao jambo ambalo si sahihi kwa kuwa chama hakina fedha za kuwanunua watu wote hao na kinachowarudisha ni kazi zinazofanyika.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Maulid Bundala, alisema vyama vya upinzani havina uwezo wa kushinda isipokuwa ushindi wao wanaupata kwa sababu ya wanachama wenyewe wa CCM ambao mchana huwa inzi na usiku hugeuka kuwa mbu.

Aliwaonya wanachama wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwa kuwa CCM ya sasa si kama ile ya zamani na wanapobaini watu kama hao wanaweza kufutwa uanachama na kuvuliwa nyadhifa walizonazo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here