30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Madereva malori watakiwa kuchukua tahadhari

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM 

SERIKALI imewataka madereva wa malori nchini kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  wakati akizungumza na baadhi ya madereva wa kampuni mbalimbali zinazosafirisha  mizigo nje ya nchi waliofika Maabara ya  Taifa ya Afya ya Jamii, Mabibo, Dar es Salaam kupima kama wana maambukizi ya virusi vya corona au laa.

Waziri Ummy alisema ugonjwa wa corona bado upo ingawa maambukizi yamepungua na kwamba jambo la muhimu ni wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya hii ikiwa ni pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa  ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na  maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu.

“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa kwa ajili ya kupima virusi vya corona, kama mtakutwa hamna maambukizi ya ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwemo machungwa, mananasi, malimao,  mboga za majani na  tangawizi, hii itawasaidia kinga zenu za mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga nyungu,’’ alisema  Ummy.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Ambele Mwafulango alisema pamoja na kupima vipimo vya wagonjwa wengine,  kwa upande wa madereva walioko Dar es Salaam kwa siku wanawapima 200 na kwa madereva walioko mikoani kuna utaratibu maalumu wa kuchukuliwa  sampuli ambazo zinatumwa Dar es Salaam kwa vipimo.

“Majibu ya vipimo yanatoka  baada ya  masaa 48, kama madereva hao  watakutwa hawana maambukzi watapewa vyeti ambavyo vinatumika kwa siku 14,  hii itawasaidia kwenda kupeleka mizigo nje ya nchi bila ya kupimwa tena katika nchi wanazokwenda,” alisema Mwafulango.

Alisema kabla madereva hao hawajafanyiwa vipimo vya corona wanapimwa joto la mwili na wale ambao watakutwa na joto la juu la mwili, watapewa huduma ya haraka zaidi ukilinganisha na wale ambao joto lao la mwili liko sawa.

“Madereva ambao tunawakuta hawana maambukizi ya ugonjwa wa corona, tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wanapokuwa safarini siku zote.

“Katika maabara hii ya Mabibo tuna mashine mpya tano ambazo ndani ya masaa 24 zinapima vipimo 1,800. Hii imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na  ilivyokuwa katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR jijini Dar es Salaam ambapo tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo 300 hadi 400 jambo ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji wetu wa kazi,’’ alisema Mwafulango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles