24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MADAKTARI WATATU WAMNUSURU MANJI KWENDA JELA

Na PATRICIA KIMELEMETA-Dar es Salaam

USHAHIDI uliotolewa na madaktari watatu katika kesi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin iliyomkabili mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji, umesababisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumwachia huru.

Akisoma hukumu iliyochukua takribani saa moja (saa 6:36 mchana hadi saa 7:37 mchana) mahakamani hapo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha, alisema kesi hiyo ilikuwa na mashahidi 10 na upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi watatu, huku upande wa Manji, ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Yanga na Mshauri wa Kampuni ya Quality Group (QG) ukiwa na mashahidi saba.

Hakimu Mkeha alisema ushahidi uliotolewa na madaktari hao, ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Profesa Mohammed Janabi, Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili na Dawa za Kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dk. Fransic Benedict na Mganga Mkuu wa Gereza la Keko, Dk. Eliud Mwakawanga, ndio uliosaidia katika hukumu ya kesi hiyo.

Hakimu Mkeha alisema katika ushahidi wake, Profesa Janabi alidai mahakamani hapo kuwa, alimpokea Manji katika Taasisi ya JKCI na kulazwa Februari na Julai, mwaka huu na kwa mara ya kwanza alipelekwa akiwa na matatizo ya moyo akiwa kama mgonjwa aliyetibiwa nje ya nchi na alirudi tena kwa mara ya pili akisumbuliwa na ugonjwa huo, huku akiwa na vyuma katika moyo wake.

Hakimu Mkeha alisema Profesa Janabi aliiambia mahakama hiyo kuwa, walimchunguza Manji kama mirija yake imeziba au haikuziba kwa sababu kazi ya vyuma ni kuzibua mishipa na walivyomchunguza wakagundua moyo wake haujakaa vizuri.

Hakimu Mkeha alisema, Profesa Janabi aliiambia mahakama hiyo kuwa Julai, mwaka huu, Manji alirudi tena JKCI akiwa na matatizo ya kupata maumivu upande wa kushoto wa mwili wake na walimwanzishia tiba.

Pia Hakimu Mkeha alisema Profesa Janabi aliiambia mahakama hiyo kuwa, Manji alipata tiba za awali katika Jimbo la Florida, nchini Marekani na wakati anafika JKCI alikuwa ametokea Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.

Hakimu Mkeha alisema Profesa Janabi alimpatia Manji dawa za aina tofauti, ila alizozikumbuka ni corvedolo, lasix na ascard na dawa nyingine kwa sababu mshtakiwa huyo pia alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kutokulala vizuri na maumivu ya mgongo na alipewa dripu ya paracetamol.

Hakimu Mkeha alisema Profesa Janabi aliiambia mahakama hiyo kuwa, Manji alikuwa na vyuma, lakini alidai kuwa kabla ya mgonjwa kuwekewa vyuma kuna vitu anakatazwa kutumia, ikiwamo sigara na heroin, ila uamuzi ni wa mgonjwa na si daktari na endapo atatumia dawa za kulevya, athari zake ni kuziba tena kwa mishipa na kusababisha operesheni kubwa zaidi ya moyo.

Hakimu Mkeha alisema shahidi mwingine katika kesi hiyo ni Dk. Mwakawanga, aliyeieleza mahakama hiyo kuwa, kuna wakati Manji alikuwa anatetemeka na wakati mwingine kama anachanganyikiwa.

Hakimu Mkeha alisema Dk. Mwakawanga aliieleza mahakama hiyo kuwa, hali ya afya ya Manji haikuwa nzuri wakati wote alipokuwa mahabusu katika gereza hilo tangu Julai 6, mwaka huu na hadi anatoka mahabusu alikuwa anatumia dawa mbalimbali na kwa siku alikuwa akinywa kati ya vidonge 25 hadi 30.

Hakimu Mkeha alisema Dk. Mwakawanga alieleza mahakamani hapo kuwa, Manji alipokelewa gerezani hapo Julai 6, mwaka huu, akitokea JKCI na hali yake ya afya haikuwa nzuri.

Hakimu Mkeha alisema Dk. Mwakawanga aliiambia mahakama hiyo kuwa, dawa zote alizokuwa anatumia Manji zilikuwa na uthibitisho wa maandishi kutoka kwa daktari wa JKCI na mshitakiwa akiwa gerezani dawa wanakaa nazo wao wataalamu na humpatia kulingana na maelekezo ya daktari.

Pia Hakimu Mkeha alisema Dk. Mwakawanga aliiambia mahakama hiyo kuwa, Manji alikunywa dawa asubuhi, jioni na nyingine mara tatu kwa siku na alikuwa na maumivu ya mgongo hadi akawa anashindwa kutembea na akawa anatumia mkanda kupunguza maumivu hayo.

Pia Hakimu Mkeha alisema kuwa, shahidi mwingine ambaye ni Dk. Francis aliiambia mahakama hiyo kuwa, ili mtu aweze kupimwa kama anatumia dawa za kulevya, lazima aache dawa anazotumia ndani ya wiki mbili, kisha ndipo apimwe, la sivyo akipimwa lazima akutwe na heroin kutokana na dawa anazotumia.

Hakimu Mkeha alisema Dk. Francis aliiambia mahakama hiyo kuwa, ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali haikuonyesha ni kiasi gani cha heroin kilichokutwa katika mkojo wa Manji.

Katika hatua nyingine, Hakimu Mkeha alisema Manji mwenyewe katika utetezi wake aliiambia mahakama hiyo kuwa, dawa zilizotajwa katika hati ya mashtaka ambazo ni morphine na benzodiazepines ni sehemu ya dawa zake anazotumia.

Hakimu Mkeha alisema Manji aliieleza mahakama hiyo kuwa, alitumia dawa hizo hata siku alipohojiwa polisi na kitendo cha kuambiwa anatumia dawa za kulevya kimemfanya achafuliwe katika jamii.

Hakimu Mkeha alisema Manji alizitaja aina ya dawa anazotumia kuwa ni aderall, vicoean, bercoced, xanax na zyban na alidai kuwa, aderal ni kwa ajili ya kuzuia kumbukumbu zisipotee kwa sababu akifanya kazi huwa akili yake inahama.

Pia Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo ilikuwa kitaalamu zaidi kuliko kisheria, kutokana na jalada alilofunguliwa Manji la matumizi ya dawa za kulevya na alipaswa kuwa makini ili kupitia ushahidi.

Alisema kutokana na hali hiyo, mahakama hiyo ilimwachia huru chini ya kifungu cha 235 cha mwenendo wa makosa ya jinai (CPA).

Alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama hiyo ilijiridhisha pasi na shaka kwamba Manji hana hatia kwa sababu upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha kosa lake.

“Mahakama imemwachia huru mfanyabiashara Yusufu Manji katika kesi iliyokuwa inamkabili ya matumizi ya dawa za kulevya baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, ambapo upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa lake,” alisema Mkeha.

Katika kesi hiyo, Manji alikuwa anatetewa na Mawakili Hudson Ndusyepo na Hajra Mungula, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Nassoro Katuga na Patrick Mwita.

Akizungumza baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Mungula alisema wamepokea vizuri hukumu hiyo kwa sababu imesomwa kwa mtiririko mzuri.

Alisema kesi ni mapambano na anashukuru wameshinda na wamefurahia hukumu hiyo.

“Hukumu tumeipokea vizuri, ila kuna mambo mengi katika hukumu, acha tukaipitie kwanza kama kuna kitu kingine nitawajulisha,” alisema Wakili Mungula.

Manji, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mbagala (CCM), ni miongoni mwa watu waliotajwa Februari 6, mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika orodha ya pili ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kuwataka wote waliotajwa kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) kwa ajili ya kuhojiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles